Habakuki 2:1-20
Habakuki 2:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi nitasimama mahali pa kuchungulia, na kukaa juu mnarani; nitakaa macho nione ataniambia nini, atajibu nini kuhusu lalamiko langu.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akanijibu hivi: “Yaandike maono haya; yaandike wazi juu ya vibao, anayepitia hapo apate kuyasoma. Maono haya yanangoja wakati wa kufaa; ni maono ya ukweli juu ya mwisho. Kama yaonekana kuchelewa, uyasubiri; hakika yatafika, wala hayatachelewa. Andika: ‘Waangalie wenye kiburi, hao wataangamia; lakini waadilifu wataishi kwa kumwamini Mungu.’” Zaidi ya hayo, divai hupotosha; mtu mwenye kiburi hatadumu. Yuko tayari kuwameza wengine kama Kuzimu; kama vile kifo, hatosheki na kitu. Hujikusanyia mataifa yote, na watu wote kama mali yake. Kila mtu atamdhihaki mtu wa namna hiyo na kumtungia misemo ya dhihaka: “Ole wako unayejirundikia visivyo vyako, na kuchukua rehani mali za watu lakini hulipi! Utaendelea kufanya hivyo hadi lini? Siku moja wadeni wako watainuka ghafla, wale wanaokutetemesha wataamka. Ndipo utakuwa mateka wao. Wewe umeyapora mataifa mengi, lakini wote wanaosalimika watakupora wewe, kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia, naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote. “Ole wako unayejitajirisha kwa hasara ya mwingine, ujengaye nyumba yako juu milimani ukidhani kuwa salama mbali na madhara. Lakini kwa mipango yako umeiaibisha jamaa yako. Kwa kuyaangamiza mataifa mengi, umeyaangamiza maisha yako mwenyewe. Ndiyo maana hata mawe yatalalamika ukutani, na boriti za nyumba zitayaunga mkono. “Ole wako unayejenga mji kwa mauaji unayesimika jiji kwa maovu! Mwenyezi-Mungu wa majeshi husababisha juhudi za watu zipotelee motoni, na mataifa yajishughulishe bure. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu utaenea pote duniani, kama vile maji yaeneavyo baharini. Ole wako unayewalewesha jirani zako, na kutia sumu katika divai yao ili upate kuwaona wamekaa uchi. Utajaa aibu badala ya heshima. Utakunywa wewe mwenyewe na kupepesuka! Mwenyezi-Mungu mwenyewe atakulevya, na aibu itaifunika heshima yako! Maovu uliyoitenda Lebanoni yatakuvamia wewe; uliwaua wanyama, wanyama nao watakutisha. Yote hayo yatakupata wewe, kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia, naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote. “Chafaa nini kinyago alichotengeneza mtu? Sanamu ni madini yaliyoyeyushwa, ni kitu cha kueneza udanganyifu! Mtengeneza sanamu hutumaini alichotengeneza mwenyewe, kinyago ambacho hakiwezi hata kusema! Ole wake mtu aliambiaye gogo: ‘Amka!’ Au jiwe bubu ‘Inuka!’ Je, sanamu yaweza kumfundisha mtu? Tazama imepakwa dhahabu na fedha, lakini haina uhai wowote.” Lakini Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu; dunia yote na ikae kimya mbele yake.
Habakuki 2:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu kuhusu kulalamika kwangu. BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake. Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu. Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani! Je! Hawatainuka ghafla wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao? Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kiota chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu! Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako. Kwa maana jiwe litapiga kelele katika ukuta, nayo boriti katika miti italijibu. Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu! Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa BWANA wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili? Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari. Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao! Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kulia wa BWANA kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako. Kwa maana udhalimu uliotendwa juu ya Lebanoni utakufunikiza, na kuangamizwa kwao wanyama kutakutia hofu; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. Sanamu ya kuchonga yafaa nini, baada ya aliyeifanya ameichonga? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema? Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa. Lakini BWANA yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.
Habakuki 2:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake. Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu. Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani! Je! Hawatainuka ghafula wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao? Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu! Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako. Kwa maana jiwe litapiga kelele katika ukuta, nayo boriti katika miti italijibu. Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu! Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa BWANA wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili? Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari. Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao! Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kuume wa BWANA kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako. Kwa maana udhalimu uliotendwa juu ya Lebanoni utakufunikiza, na kuangamizwa kwao wanyama kutakutia hofu; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. Sanamu ya kuchora yafaa nini, hata yeye aliyeifanya ameichora? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema? Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa. Lakini BWANA yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.
Habakuki 2:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nitasimama katika zamu yangu, na kujiweka juu ya maboma; nitatazama nione atakaloniambia, na jibu nitakalotoa kuhusu lalamiko hili. BWANA Kisha BWANA akajibu: “Andika ufunuo huu, na ukaufanye wazi juu ya vibao, ili mpiga mbiu akimbie nao. Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika; unazungumzia mambo ya mwisho, na kamwe hautakosea. Iwapo utakawia, wewe usubiri; kwa hakika utakuja na hautachelewa. “Tazama, amejaa majivuno; anavyovitamani si vya unyofu: lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake: hakika mvinyo humsaliti; ni mwenye kiburi na hana amani. Kwa sababu ni mlafi kama Kuzimu, na kama kifo kamwe hatosheki; anajikusanyia mataifa yote na kuchukua watu wote mateka. “Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema, “ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu! Ataendelea hivi kwa muda gani?’ Je, wadai wako hawatainuka ghafula? Je, hawataamka na kukufanya utetemeke? Kisha utakuwa mhanga kwao. Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi, watu waliobaki watakuteka nyara wewe. Kwa kuwa umemwaga damu ya watu; umeharibu nchi na miji, na watu wote wanaoishi humo. “Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu, awekaye kiota chake juu, ili kukimbia makucha ya uharibifu! Umepanga njama ya maangamizi ya watu wengi, ukiaibisha nyumba yako mwenyewe, na kupotewa na maisha yako. Mawe ya kuta yatapiga kelele, na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake. “Ole wake yeye ajengaye mji kwa kumwaga damu na kuusimamisha mji kwa uhalifu! Je, BWANA wa majeshi hakuonesha kwamba kazi ya wanadamu ni mafuta tu kwa ajili ya moto, na kwamba mataifa yanajichosha bure? Kwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari. “Ole wake yeye awapaye majirani zake kileo, akikimimina kutoka kwa kiriba cha mvinyo hadi wamelewa, ili apate kutazama miili yao iliyo uchi. Utajazwa na aibu badala ya utukufu. Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue! Kikombe kutoka mkono wa kuume wa BWANA kinakujia, na aibu itafunika utukufu wako. Ukatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika, na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha. Kwa sababu umemwaga damu ya mtu; umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliye ndani yake. “Sanamu ina thamani gani, kwani mwanadamu ndiye alichonga? Ama kinyago kinachofundisha uongo? Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe; hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza. Ole wake yeye auambiaye mti, ‘Uwe hai!’ Ama asemaye na jiwe lisilo na uhai, ‘Amka!’ Je, linaweza kuongoza? Limefunikwa kwa dhahabu na fedha; hakuna pumzi ndani yake. Lakini BWANA yuko katika Hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze mbele yake.”