Habakuki 1:1-6
Habakuki 1:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Kauli ya Mungu aliyoiona nabii Habakuki. “Ee Mwenyezi-Mungu, nitakulilia mpaka lini, nawe usinisikilize na kunisaidia? Kwa nini nalia: ‘Dhuluma’ nawe hutuokoi? Kwa nini wanifanya nishuhudie mabaya na taabu? Uharibifu na ukatili vinanizunguka, ugomvi na mashindano yanazuka. Hivyo sheria haina nguvu, wala haki haitekelezwi. Waovu wanawazunguka waadilifu, hivyo hukumu hutolewa ikiwa imepotoshwa.” Mungu akasema: “Yaangalie mataifa, uone! Utastaajabu na kushangaa. Maana ninatenda kitu ukiwa bado unaishi, kitu ambacho ungeambiwa hungesadiki. Maana ninawachochea Wakaldayo, taifa lile kali na lenye hamaki! Taifa lipitalo katika nchi yote, ili kunyakua makao ya watu wengine.
Habakuki 1:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo aliouona nabii Habakuki. Ee BWANA, nilie hadi lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. Mbona wanionesha uovu, na kunifanya nione mabaya? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu inayotolewa huwa imepotoshwa. Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa. Kwa maana, angalieni, nawachochea Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.
Habakuki 1:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo aliouona nabii Habakuki. Ee BWANA, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka. Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa. Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.
Habakuki 1:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la unabii alilopokea nabii Habakuki. Ee BWANA, hata lini nitakuomba msaada, lakini wewe husikilizi? Au kukulilia, “Udhalimu!” lakini hutaki kuokoa? Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma? Kwa nini unavumilia makosa? Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu; kuna mabishano na mapambano kwa wingi. Kwa hiyo sheria imepotoshwa, nayo haki haipo kabisa. Waovu wanawazunguka wenye haki, kwa hiyo haki imepotoshwa. BWANA “Yatazame mataifa, uangalie na ushangae kabisa. Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu ambacho hungeamini, hata kama ungeambiwa. Tazama! Nitawainua Wakaldayo, watu wakatili na wenye haraka, ambao hupita dunia yote ili kuteka makazi yasiyo yao.