Mwanzo 8:1-19
Mwanzo 8:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua. Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa, maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana. Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arubaini, Noa alifungua dirisha alilokuwa ametengeneza katika hiyo safina, akamtoa kunguru nje, naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini. Kisha Noa akamtoa njiwa apate kuona kama maji yalikuwa yamepungua juu ya nchi. Lakini, kwa vile maji yalikuwa bado yameifunika nchi yote, huyo njiwa hakupata mahali pa kutua, akamrudia Noa katika safina. Noa akanyosha mkono, akamtwaa na kumrudisha ndani ya safina. Noa akangoja siku nyingine saba, kisha akamtoa tena huyo njiwa. Njiwa huyo akamrudia Noa saa za jioni akiwa na tawi bichi la mzeituni mdomoni mwake. Kwa hiyo Noa akajua kwamba maji yalikuwa yamepungua katika nchi. Kisha akangoja siku nyingine saba, akamtoa tena yule njiwa; safari hii njiwa hakurudi kabisa. Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka. Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa. Hapo, Mungu akamwambia Noa, “Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.” Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe. Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani.
Mwanzo 8:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia moja na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakapungukapunguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. Ikawa baada ya siku arubaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huku na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelichuma, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa makabila yao, wakatoka katika safina.
Mwanzo 8:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina.
Mwanzo 8:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mungu akamkumbuka Nuhu na wanyama pori na mifugo wote waliokuwa naye ndani ya safina; akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakapungua. Chemchemi za vilindi zikawa zimefungwa, na malango ya mafuriko ya mbinguni pia yakawa yamefungwa; nayo mvua ikawa imekoma kunyesha. Maji yakaendelea kupungua taratibu katika dunia. Mwishoni mwa siku ya mia moja na hamsini, maji yakawa yamepungua. Na katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu. Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. Kufikia siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili, dunia ilikuwa imekauka kabisa. Ndipo Mungu akamwambia Nuhu, “Toka katika safina, wewe na mkeo, na wanao na wake zao. Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe, wakiwamo ndege, wanyama na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.” Kwa hiyo Nuhu akatoka nje pamoja na mkewe, na wanawe na wake zao. Wanyama wote na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, na ndege wote, kila kitu kinachoenda juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina.