Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 46:1-34

Mwanzo 46:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Israeli akaanza safari yake pamoja na mali yake yote. Alipofika Beer-sheba, akamtolea tambiko Mungu wa Isaka, baba yake. Mungu akaongea na Israeli katika maono usiku, akamwita, “Yakobo! Yakobo!” Yakobo akaitika, “Naam nasikiliza.” Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kwenda Misri; utakapokuwa huko, nitakufanya uwe taifa kubwa. Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe huko Misri na kukurudisha huku. Utakapofariki, mkono wa Yosefu ndio utakaoyafumba macho yako.” Basi, Yakobo akaondoka Beer-sheba. Wanawe wakamchukua yeye, watoto wao wachanga pamoja na wake zao katika magari ambayo Farao alipeleka kumchukua. Walichukua pia mifugo na mali yao yote waliyokuwa wamechuma katika nchi ya Kanaani, wakaenda Misri. Yakobo aliwachukua wazawa wake wote: Wanawe, wajukuu wake wa kiume na wa kike, wote akawaleta Misri. Wazawa wa Israeli ambao walikwenda Misri pamoja naye walikuwa Reubeni, mzaliwa wake wa kwanza, pamoja na wana wa Reubeni: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Simeoni na wanawe: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli, aliyezaliwa na mwanamke Mkanaani. Lawi na wanawe: Gershoni, Kohathi na Merari. Yuda na wanawe: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera. (Lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi walikuwa Hesroni na Hamuli. Isakari na wanawe: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni. Zebuluni na wanawe: Seredi, Eloni na Yaleeli. Hao ndio wana ambao Lea alimzalia Yakobo kule Padan-aramu, pamoja na Dina binti yake. Jumla ya wanawe, binti zake na wajukuu wake walikuwa watu thelathini na watatu. Gadi na wanawe: Sifioni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli. Asheri na wanawe: Imna, Ishva, Ishvi, Beria na Sera, dada yao. Beria na wanawe: Heberi na Malkieli. Hawa kumi na sita ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Zilpa, mjakazi ambaye Labani alimpa Lea, binti yake. Raheli alimzalia Yakobo wana wawili: Yosefu na Benyamini. Huko Misri, Asenathi, binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili: Manase na Efraimu. Wana wa Benyamini walikuwa Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi. Watu hao kumi na wanne ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Raheli, mkewe. Dani na Hushimu, mwanawe. Naftali na wanawe: Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu. Hao saba ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Bilha, mjakazi ambaye Labani alimpa binti yake Raheli. Jumla ya wazawa wa Yakobo aliokwenda nao Misri, bila kuwahesabu wake za wanawe, ilikuwa watu sitini na sita. Huko nchini Misri Yosefu alikuwa amepata wana wawili. Kwa hiyo watu wote wa jamaa ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akamtanguliza Yuda kwa Yosefu kumwomba waonane huko Gosheni; nao wakafika katika eneo la Gosheni. Yosefu akapanda gari lake la farasi, akaenda kumlaki Israeli, baba yake, huko Gosheni. Alipomfikia baba yake, alimkumbatia na kulia kwa kitambo kirefu. Israeli akamwambia Yosefu, “Hata nikifa sasa si kitu kwa kuwa nimeuona uso wako na kujua kwamba wewe u hai!” Yosefu akawaambia ndugu zake na jamaa yote ya baba yake, “Nakwenda kumwarifu Farao kwamba ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu waliokuwa katika nchi ya Kanaani wamekuja kwangu. Nitamweleza kwamba nyinyi ni wachungaji kwani mmekuwa mkichunga mifugo, na kwamba mmewasili pamoja na mbuzi, kondoo, ng'ombe na mali yenu yote. Basi, Farao akiwaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ Semeni: ‘Bwana, sisi watumishi wako, ni wafugaji wa mifugo tangu utoto wetu mpaka leo, kwani ndivyo walivyokuwa babu zetu’; semeni hivyo ili mruhusiwe kukaa katika eneo la Gosheni.” Yosefu alisema hivyo kwa sababu kwa Wamisri wachungaji wote wa kondoo ni chukizo.

Shirikisha
Soma Mwanzo 46

Mwanzo 46:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Israeli Akasafiri, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyotuma Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamepata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri. Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi. Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani. Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari. Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli. Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni. Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli. Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Wanawe wote wa kiume na kike walikuwa watu thelathini na watatu. Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli. Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, dada yao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli. Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, watu kumi na sita. Wana wa Raheli, mkewe Yakobo, Yusufu na Benyamini. Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni. Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi. Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, wote walikuwa watu kumi na wanne. Na wana wa Dani; Hushimu. Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu. Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; wote walikuwa watu saba. Watu wote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri, waliokuwa wazawa wake, bila wake za wanawe, walikuwa watu sitini na sita. Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa wawili. Watu wote wa nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akamtuma Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kirefu. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai. Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumishi wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 46

Mwanzo 46:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri. Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi. Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani. Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari. Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli. Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni. Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli. Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Nafsi zote za wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu. Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli. Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, umbu lao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli. Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, nafsi kumi na sita. Wana wa Raheli, mkewe Yakobo Yusufu na Benyamini. Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni. Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi. Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, nafsi zote walikuwa kumi na wanne. Na wana wa Dani; Hushimu. Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu. Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; nafsi zote walikuwa saba. Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita. Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai. Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng’ombe zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 46

Mwanzo 46:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hivyo Israeli akaondoka na mali yake yote. Alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaka baba yake. Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!” Akamjibu, “Mimi hapa.” Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako. Usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yusufu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.” Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba, nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo, na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao alikuwa amempelekea kumsafirisha. Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani; Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote hadi Misri. Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), walioenda Misri: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Wana wa Reubeni ni: Hanoki, Palu, Hesroni, na Karmi. Wana wa Simeoni ni: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. Wana wa Lawi ni: Gershoni, Kohathi, na Merari. Wana wa Yuda ni: Eri, Onani, Shela, Peresi, na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi ni: Hesroni na Hamuli. Wana wa Isakari ni: Tola, Puva, Yashubu, na Shimroni. Wana wa Zabuloni ni: Seredi, Eloni, na Yaleeli. Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu, pamoja na binti yake Dina. Jumla ya hawa wanawe wa kiume na wa kike walikuwa thelathini na watatu. Wana wa Gadi ni: Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi, na Areli. Wana wa Asheri ni: Imna, Ishva, Ishvi, na Beria. Dada yao alikuwa Sera. Wana wa Beria ni: Heberi na Malkieli. Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita. Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni: Yusufu na Benyamini. Huko Misri, Asenathi binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili: Manase na Efraimu. Wana wa Benyamini ni: Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu, na Ardi. Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne. Mwana wa Dani ni: Hushimu. Wana wa Naftali ni: Yaseeli, Guni, Yeseri, na Shilemu. Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba. Wote walioenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe wake, walikuwa watu sitini na sita. Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla ya jamaa ya Yakobo walioenda Misri walikuwa sabini. Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, Yusufu aliandaa gari lake la vita, na akaenda Gosheni kumlaki baba yake, Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu. Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.” Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, walioishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. Watu hao ni wafugaji; wao huchunga mifugo, na wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho.’ Farao atakapowaita na kuwauliza, ‘Kazi yenu ni nini?’ mjibuni, ‘Watumishi wako wamekuwa wafugaji wa wanyama tangu ujana wetu hadi sasa, kama baba zetu walivyokuwa.’ Ndipo mtaruhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wafugaji wote ni chukizo kwa Wamisri.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 46