Mwanzo 45:4-7
Mwanzo 45:4-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa.
Mwanzo 45:4-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinituma mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo ya kulima wala kuvuna. Mungu alinituma mbele yenu kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.
Mwanzo 45:4-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.
Mwanzo 45:4-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yusufu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa njaa imekuwa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwa na kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.