Mwanzo 41:46-57
Mwanzo 41:46-57 Biblia Habari Njema (BHN)
Yosefu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kumtumikia Farao, mfalme wa Misri. Alitoka nyumbani kwa Farao na kuitembelea nchi yote ya Misri. Ikawa, katika miaka ile saba ya shibe, mashamba ya Misri yakatoa mazao kwa wingi sana. Yosefu akakusanya chakula chote wakati huo wa miaka saba ya shibe na kukiweka akiba katika miji ya Misri. Katika kila mji akaweka akiba ya chakula kutoka mashamba yaliyo karibu na mji huo. Yosefu akaweka akiba ya nafaka kwa wingi mno ikawa nyingi kama mchanga wa bahari, hata isiweze kupimika. Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Yosefu alikuwa amekwisha pata wana wawili kwa mkewe, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Yosefu alimwita mwanawe wa kwanza Manase, akisema, “Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote na jamaa ya baba yangu.” Mwanawe wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Mungu amenipa watoto katika nchi ya mateso yangu.” Miaka ile saba ya shibe nchini Misri ikapita. Ikaanza miaka saba ya njaa kama alivyokuwa amesema Yosefu hapo awali. Nchi nyingine zote zikawa na njaa, lakini nchi yote ya Misri ilikuwa na chakula. Wakati wananchi wa Misri walipoanza kuona njaa, walimlilia Farao awape chakula. Naye Farao akawaambia Wamisri wote, “Nendeni kwa Yosefu; atakalowaambia fanyeni.” Njaa ikazidi kuwa kali na kuenea katika nchi yote. Kwa hiyo Yosefu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri chakula. Zaidi ya hayo, watu toka kila mahali duniani walikuja Misri kwa Yosefu kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa kali duniani kote.
Mwanzo 41:46-57 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akasafiri katika nchi yote ya Misri. Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ilitoa mazao mengi kabla ya kuja kwa miaka ya njaa. Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake. Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu. Kabla ya kuja miaka ya njaa, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili. Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu. Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu. Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri, ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula. Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Nendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.
Mwanzo 41:46-57 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri. Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi. Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake. Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu. Kabla ya kuja miaka ya njaa, Yusufu akazaliwa wana wawili, ambao Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia. Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu. Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu. Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri, ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula. Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.
Mwanzo 41:46-57 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yusufu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao, mfalme wa Misri. Naye Yusufu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. Katika ile miaka saba ya shibe nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. Yusufu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya shibe nchini Misri, akakihifadhi katika miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. Yusufu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari; ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi kipimo. Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili wa kiume. Yusufu akamwita mzaliwa wake wa kwanza jina Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” Mwana wa pili akamwita jina Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.” Ile miaka saba ya shibe huko Misri ikaisha, nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yusufu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. Nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao aliwaagiza Wamisri wote, “Nendeni kwa Yusufu, nanyi mfanye anachowaambia.” Njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yusufu akafungua maghala ya vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yusufu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.