Mwanzo 41:14-32
Mwanzo 41:14-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Farao akaamuru Yosefu aitwe; naye akatolewa gerezani haraka. Baada ya kunyoa na kubadili nguo zake, Yosefu akaja mbele ya Farao. Farao akamwambia Yosefu, “Mimi nimeota ndoto, lakini hakuna mtu aliyeweza kunitafsiria. Nimesikia sifa zako kwamba wewe ukiambiwa ndoto unaweza kuitafsiri.” Yosefu akamjibu Farao, “Sina uwezo huo; lakini Mungu atakupa jibu lifaalo.” Hapo Farao akamwambia Yosefu, “Niliota kwamba nimesimama kando ya mto Nili, nikaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. Hao wakafuatwa na ng'ombe wengine saba dhaifu, wembamba na wamekonda sana. Mimi sijapata kamwe kuona ng'ombe wa hali hiyo katika nchi ya Misri. Basi, wale ng'ombe waliokonda sana wakawala wale ng'ombe saba wanono. Lakini hata baada ya kuwala wale wanono, mtu yeyote asingeweza kutambua kwamba wamewala wenzao, kwani bado walikuwa wamekondeana kama mwanzo. Hapo nikaamka usingizini. Kisha nikaota ndoto nyingine: Niliona masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka yakichipua katika bua moja. Halafu yakafuatwa na masuke mengine saba matupu, membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani. Yale masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba mazuri. Basi, mimi niliwaambia wachawi ndoto hizo lakini hakuna mtu aliyeweza kunifafanulia.” Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto zako zote mbili tafsiri yake ni moja. Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. Ngombe wale saba wazuri ni miaka saba, na yale masuke saba mazuri pia ni miaka saba; ndoto hiyo tafsiri yake ni moja. Wale ng'ombe saba waliokonda sana, ambao waliwafuata wale wanono, na yale masuke matupu saba, yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani, maana yake ni miaka saba ya njaa. Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri. Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii. Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni.
Mwanzo 41:14-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Farao akatuma watu kumwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa mto; na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha nyasini. Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipowala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionesha maana yake. Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa kali sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.
Mwanzo 41:14-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto; na tazama, ng’ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini. Kisha, tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng’ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng’ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake. Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng’ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng’ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.
Mwanzo 41:14-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi, Farao akatuma Yusufu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake, akaenda mbele ya Farao. Farao akamwambia Yusufu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia habari yako kwamba unapoelezwa ndoto unaweza kuifasiri.” Yusufu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.” Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili. Nikawaona ngʼombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni, wakaja kujilisha kwenye matete. Baada ya hao, ngʼombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ngʼombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. Hao ngʼombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ngʼombe saba walionona waliojitokeza kwanza. Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini. “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. Baada ya hayo, masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.” Ndipo Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto hiyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Ngʼombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba; ni ndoto hiyo hiyo moja. Ngʼombe saba waliokonda na wabaya waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki: Ni miaka saba ya njaa. “Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri, lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi. “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.