Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 39:1-12

Mwanzo 39:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Yosefu alipochukuliwa mpaka Misri, Mmisri mmoja aitwaye Potifa ambaye alikuwa ofisa wa Farao na mkuu wa kikosi chake cha ulinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri. Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri. Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu. Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote. Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani. Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe. Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza. Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”. Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena. Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.” Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe. Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani. Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje.

Shirikisha
Soma Mwanzo 39

Mwanzo 39:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri, naye Potifa, ofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Baraka za BWANA zikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nimkosee Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala kuwa naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani afanye kazi yake, na hapakuwa na mtu yeyote kati ya wale wa nyumbani karibu; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.

Shirikisha
Soma Mwanzo 39

Mwanzo 39:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.

Shirikisha
Soma Mwanzo 39

Mwanzo 39:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Wakati huu Yusufu alikuwa amechukuliwa hadi Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, na aliyekuwa mkuu wa walinzi, akamnunua Yusufu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri. BWANA alikuwa pamoja na Yusufu, naye akastawi. Yusufu akaishi nyumbani mwa bwana wake Mmisri. Potifa alipoona kuwa BWANA alikuwa pamoja na Yusufu, na kwamba BWANA alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, Yusufu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamweka kuwa mwangalizi wa mali yake yote. Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yusufu kuwa msimamizi wa nyumba na mali yake yote aliyokuwa nayo, BWANA aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yusufu. Baraka ya BWANA ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. Kwa hiyo Potifa akamwachia Yusufu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. Yusufu alipokuwa msimamizi wa mali yake, Potifa hakujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula. Yusufu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia. Baada ya kitambo, mke wa Potifa akamtamani Yusufu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!” Lakini Yusufu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa msimamizi, bwana wangu hajishughulishi na kitu chochote katika nyumba hii; kila kitu alicho nacho amenikabidhi. Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yusufu siku baada ya siku, Yusufu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye. Siku moja Yusufu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwa mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. Mke wa Potifa akashika vazi Yusufu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yusufu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 39