Mwanzo 37:1-36
Mwanzo 37:1-36 Biblia Habari Njema (BHN)
Yakobo aliendelea kukaa katika nchi ya Kanaani, alimoishi baba yake kama mgeni. Hizi ndizo habari za ukoo wa Yakobo. Yosefu, akiwa kijana wa umri wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, wana wa Bilha na Zilpa, wake za baba yake. Yosefu akawa anamjulisha baba yake juu ya tabia mbaya za ndugu zake. Israeli alimpenda Yosefu kuliko watoto wake wote kwa sababu alikuwa amezaliwa wakati wa uzee wake. Alimshonea Yosefu kanzu ndefu. Lakini ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda Yosefu kuliko wao, wakamchukia hata hawakuzungumza naye kwa amani. Usiku mmoja, Yosefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia. Aliwaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: Niliota kuwa sote tulikuwa shambani tukifunga miganda na ghafla mganda wangu ukainuka na kusimama wima. Miganda yenu ikakusanyika kuuzunguka na kuuinamia mganda wangu.” Ndugu zake wakamwuliza, “Je, unataka kutuambia kwamba utatutawala? Au utakuwa na mamlaka juu yetu?” Basi, wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto na maneno yake. Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.” Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?” Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo. Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu. Basi, Israeli akamwambia Yosefu, “Unajua ndugu zako wanachunga wanyama kule Shekemu. Kwa hiyo nataka nikutume kwao.” Yosefu akajibu, “Niko tayari.” Baba yake akamwambia, “Nenda ukawaangalie ndugu zako na wanyama kama wako salama, kisha uniletee habari.” Basi, Yakobo akamtuma Yosefu kutoka bonde la Hebroni. Yosefu alipokaribia Shekemu mtu mmoja akamkuta akitangatanga mbugani, akamwuliza, “Unatafuta nini?” Yosefu akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali, niambie mahali wanakochunga wanyama.” Yule mtu akamwambia, “Bila shaka wamekwisha ondoka, kwa sababu niliwasikia wakisema kwamba wanakwenda Dothani.” Basi, Yosefu akawafuata ndugu zake, akawakuta huko Dothani. Ndugu zake walipomwona akiwa mbali na kabla hajafika karibu, wakafanya mpango wa kumuua. Waliambiana, “Tazameni! Yule mwota ndoto anakuja. Haya, tumuue na kumtupa ndani ya shimo mojawapo. Baadaye tutasema kwamba ameuawa na mnyama wa porini. Halafu tutaona hizo ndoto zake zitakuwaje.” Lakini Reubeni aliposikia maneno hayo, akataka kumwokoa mikononi mwao; basi akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, tusimuue. Msimwage damu. Ila mtumbukizeni katika shimo hili hapa mbugani, lakini msimdhuru.” Alisema hivyo kusudi aweze kumwokoa Yosefu mikononi mwao, na baadaye amrudishe kwa baba yake. Yosefu alipowafikia ndugu zake, wao wakamvua kanzu yake. Kisha wakamshika na kumtupa shimoni. Lakini shimo hilo halikuwa na maji. Walipoketi kula, wakaona msafara wa Waishmaeli wakisafiri kutoka Gileadi kwenda Misri. Ngamia wao walikuwa wamebeba ubani, zeri na manemane. Hapo Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutapata faida gani tukimuua ndugu yetu na kuficha mauaji yake? Afadhali tumwuze kwa hawa Waishmaeli, lakini tusiguse maisha yake, kwani yeye ni ndugu yetu; yeye ni damu moja nasi.” Ndugu zake wakakubaliana naye. Wafanyabiashara Wamidiani walipofika mahali hapo, hao ndugu wakamtoa Yosefu katika shimo, wakamwuza kwa Waishmaeli kwa bei ya vipande ishirini vya fedha; nao wakamchukua Yosefu hadi Misri. Basi, Reubeni aliporudi kwenye lile shimo, na asimwone Yosefu tena, akazirarua nguo zake kwa huzuni, akawaendea ndugu zake, akawaambia, “Kijana hayupo nami niende wapi?” Basi, wakachinja mbuzi, wakaichukua kanzu ya Yosefu na kuichovya katika damu ya huyo mbuzi. Kisha wakampelekea baba yao ile kanzu, wakamwambia, “Tumeiokota kanzu hii. Hebu iangalie kama ni ya mwanao, au siyo.” Baba yao akaitambua hiyo kanzu, akasema, “Ndiyo hasa! Bila shaka mnyama wa porini amemshambulia na kumla. Hakika Yosefu ameraruliwa vipandevipande.” Hapo Yakobo akayararua mavazi yake kwa huzuni, akavaa vazi la gunia kiunoni. Akamlilia mwanawe kwa muda wa siku nyingi. Watoto wake wa kiume na wa kike wakamjia ili kumfariji, lakini akakataa kufarijiwa, akisema, “Niacheni; nitaendelea kuomboleza kwa ajili ya mwanangu, mpaka nitakaposhuka kuzimu alipo.” Ndivyo baba yake alivyomlilia. Wakati huo, kule Misri, wale Wamidiani walimwuza Yosefu kwa mtu aitwaye Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi.
Mwanzo 37:1-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie mpaka chini? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia, Nenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akamtuma kutoka bonde la Hebroni, na akafika Shekemu. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazungukazunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona akiwa mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika shimo mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika shimo hili lililopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika shimo; na hilo shimo ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya, na tumuuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika shimo, wakamuuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitashuka kaburini kwa mwanangu, nikiomboleza. Basi baba yake akamlilia. Nao Wamidiani wakamuuza huko Misri, kwa Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi.
Mwanzo 37:1-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia. Nao Wamidiani wakamwuza huko Misri, kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari.
Mwanzo 37:1-36 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi. Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, yaani wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake za baba yake, naye akamletea baba yao taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko ndugu zake wote, kwa sababu alikuwa mwanawe wa uzeeni; akamshonea joho lililofumwa vizuri sana. Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yusufu kuliko yeyote kati yao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema. Yusufu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani. Ghafula mganda wangu ukasimama wima, nayo miganda yenu ikauzunguka na kuuinamia.” Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto yake, pamoja na yale aliyowaambia. Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akisema, “Sikilizeni: nimeota ndoto nyingine. Wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.” Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako, na mimi, na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe?” Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni. Basi ndugu zake walikuwa wameenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.” Yusufu akajibu, “Vema sana, niko tayari.” Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama ndugu zako wako salama, na makundi pia, kisha uniletee habari.” Basi akamtuma Yusufu kutoka Bonde la Hebroni. Yusufu alipofika Shekemu, mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani, akamuuliza, “Unatafuta nini?” Akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?” Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twendeni Dothani.’ ” Kwa hiyo Yusufu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani. Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga njama za kumuua. Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo, na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.” Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao, akasema, “Tusimuue. Msimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani mwa baba yake. Kwa hiyo Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililofumwa vizuri alilokuwa amevaa. Kisha wakamchukua, wakamtupa katika shimo. Hilo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji. Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini tukimuua ndugu yetu na kuificha damu yake? Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, mwili wetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali. Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yusufu kutoka lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri. Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yusufu hayupo, alirarua nguo zake. Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?” Kisha wakalichukua lile joho la Yusufu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. Wakalichukua lile joho lililofumwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.” Baba yao akalitambua, akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yusufu ameraruliwa vipande vipande.” Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. Wanawe wote wa kiume na wa kike wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu hadi nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia. Basi Wamidiani wakamuuza Yusufu huko Misri kwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa walinzi.