Mwanzo 33:12-20
Mwanzo 33:12-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.” Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa. Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.” Hapo Esau akasema, “Heri nikuachie baadhi ya watu wangu.” Lakini Yakobo akasema, “Kuna haja gani ya kufanya hivyo? Yanitosha kwamba mimi nimepata fadhili yako, ewe bwana wangu.” Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri. Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukothi, na huko akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo, mahali hapo pakaitwa Sukothi. Kutoka Padan-aramu, Yakobo alifika salama mjini Shekemu, katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi yake karibu na mji huo. Sehemu hiyo ya ardhi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazawa wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. Huko, akajenga madhabahu na kupaita Mungu ni Mungu wa Israeli.
Mwanzo 33:12-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia. Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hadi nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri. Esau akasema, Basi nikuachie, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu. Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri. Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi. Yakobo akaja kwa amani mpaka katika mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji. Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia moja vya fedha. Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.
Mwanzo 33:12-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia. Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng’ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri. Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu. Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri. Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi. Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji. Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.
Mwanzo 33:12-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Esau akasema, “Tuendelee na safari; nitakusindikiza.” Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa ngʼombe na kondoo wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa. Hivyo bwana wangu, mtangulie mtumishi wako, nami nije polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, hadi nifike kwa bwana wangu huko Seiri.” Esau akamwambia, “Basi kubali nikuachie baadhi ya watu wangu.” Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo? Niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.” Hivyo siku hiyo Esau akashika njia, akarudi Seiri. Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi. Akajijengea makazi na pia vibanda vya mifugo yake. Hii ndiyo sababu mahali pale panaitwa Sukothi. Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani, na kuweka kambi yake karibu na mji huo. Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia moja vya fedha, akapiga hema lake hapo. Akajenga madhabahu pale na kupaita El-Elohe-Israeli.