Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 3:6-16

Mwanzo 3:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni. Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hivyo, umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa, na kuliko wanyama wote wa porini. Kwa tumbo lako utatambaa, na kula vumbi siku zote za maisha yako. Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzawa wako na uzawa wake; yeye atakiponda kichwa chako, nawe utamwuma kisigino chake.” Kisha akamwambia mwanamke, “Nitakuzidishia uchungu wa kuzaa, kwa uchungu utazaa watoto. Hata hivyo utakuwa na hamu na mumeo, naye atakutawala.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 3

Mwanzo 3:6-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mwanamke alipotambua kwamba tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma matunda yake, akala. Pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, akala. Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika. Yule mwanaume na mkewe waliposikia sauti ya BWANA Mungu akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka kwa BWANA Mungu katikati ya miti ya bustani. Lakini BWANA Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?” Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.” Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?” Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa matunda ya huo mti, nami nikala.” Ndipo BWANA Mungu akamuuliza mwanamke, “Umefanya jambo gani?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.” Hivyo BWANA Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko mifugo wote na wanyama pori wote! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako. Nami nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, na kati ya uzao wako na wake; yeye atakuponda kichwa, nawe utamuuma kisigino.” Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana uchungu wakati wa kuzaa kwako; kwa uchungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 3