Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 3:1-13

Mwanzo 3:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?” Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’” Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni. Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 3

Mwanzo 3:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi nyoka alikuwa mjanja kuliko wanyama pori wote ambao BWANA Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?” Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyo katika bustani, lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ” Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. Kwa maana Mungu anajua kwamba mtakapokula tunda hilo, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Mwanamke alipotambua kwamba tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma matunda yake, akala. Pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, akala. Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika. Yule mwanaume na mkewe waliposikia sauti ya BWANA Mungu akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka kwa BWANA Mungu katikati ya miti ya bustani. Lakini BWANA Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?” Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.” Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?” Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa matunda ya huo mti, nami nikala.” Ndipo BWANA Mungu akamuuliza mwanamke, “Umefanya jambo gani?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 3