Mwanzo 29:1-14
Mwanzo 29:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Yakobo aliendelea na safari yake, akafika katika nchi za watu wa mashariki. Siku moja akaona kisima mbugani, na kando yake makundi matatu ya kondoo wamepumzika. Kondoo walikuwa wananyweshwa kutoka kisima hicho kilichokuwa kimefunikwa kwa jiwe kubwa. Kwa kawaida, makundi yote ya kondoo yalipokusanyika, wachungaji walivingirisha hilo jiwe kwa pamoja toka kisimani na kuwanywesha kondoo. Halafu walikifunika tena kisima kwa jiwe hilo. Yakobo akawauliza wachungaji, “Ndugu zangu, mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.” Naye akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakamjibu, “Tunamfahamu.” Akaendelea kuwauliza, “Je, hajambo?” Nao wakamjibu, “Hajambo; hata binti yake Raheli, yule kule anakuja na kondoo wake!” Hapo Yakobo akawaambia, “Naona bado ni mchana, na si wakati wa kuwakusanya kondoo pamoja. Basi, wanywesheni kondoo maji, mwende mkawachunge.” Lakini wao wakamwambia, “Hatuwezi kufanya hivyo mpaka makundi yote yawe yamekusanyika pamoja, na jiwe limevingirishwa kisimani, ndipo tuwanyweshe kondoo.” Yakobo alipokuwa bado anazungumza na hao wachungaji, Raheli akafika na kondoo wa baba yake, kwani ndiye aliyekuwa akiwachunga. Yakobo alipomwona Raheli, bintiye Labani, kaka ya mama yake, na alipowaona kondoo wa Labani, mjomba wake, akaenda na kulivingirisha lile jiwe kwenye mdomo wa kisima, akalinywesha maji kundi la Labani, mjomba wake. Kisha Yakobo akambusu Raheli na kulia kwa sauti. Halafu Yakobo akamjulisha Raheli kuwa yeye ni wa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Raheli akapiga mbio nyumbani akamwarifu baba yake. Labani aliposikia habari za Yakobo, mpwa wake, alikwenda mbio kumlaki, akamkumbatia, akambusu, akamkaribisha nyumbani kwake. Yakobo akamsimulia Labani mambo yote yaliyotokea. Naye Labani akasema, “Hakika, wewe ni jamaa yangu, damu moja nami!” Yakobo akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja.
Mwanzo 29:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki. Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima. Makundi yote hukusanyika huko, watu wakabingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake. Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, ninyi ni watu wa wapi? Wakasema, Sisi tu wa Harani. Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. Akasema, Tazama, kungali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. Wakasema, Hatuwezi, Mpaka makundi yote yakusanyike, watu wakabingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. Na alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulibingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akalia kwa sauti. Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari. Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.
Mwanzo 29:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki. Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima. Makundi yote hukusanyika huko, watu wakafingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake. Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi. Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia. Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari. Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.
Mwanzo 29:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha Yakobo akaendelea na safari yake, na akafika nchi ya watu wa mashariki. Huko akaona kisima katika shamba, pamoja na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu na kisima hicho, kwa sababu walikuwa wakinyweshwa kutoka kisima hicho. Jiwe lililokuwa juu ya mdomo wa kisima lilikuwa kubwa. Kondoo walipokusanyika hapo, wachungaji walilivingirisha jiwe hilo kutoka mdomo wa kisima. Kisha walilirudisha jiwe mahali pake juu ya mdomo wa kisima. Yakobo aliwauliza wachungaji, “Ndugu zangu, ninyi mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.” Akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani, mjukuu wa Nahori?” Wakamjibu, “Ndiyo, tunamfahamu.” Kisha Yakobo akawauliza, “Je, yeye ni mzima?” Wakasema, “Ndiyo, ni mzima; na hapa yuaja Raheli binti yake akiwa na kondoo.” Akawaambia, “Tazama, jua bado liko juu, si wakati wa kukusanya mifugo. Nywesheni kondoo na mwarudishe malishoni.” Wakamjibu, “Haiwezekani, hadi kondoo wote wakusanyike, nalo jiwe livingirishwe kutoka mdomo wa kisima. Ndipo tutawanywesha kondoo.” Alipokuwa akizungumza nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, kwa maana alikuwa mchunga kondoo. Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mama yake, pamoja na kondoo wa Labani, alienda na kulivingirisha jiwe kutoka mdomo wa kisima na kuwanywesha kondoo wa mjomba wake. Kisha Yakobo akambusu Raheli, na akaanza kulia kwa sauti. Yakobo alikuwa amemwambia Raheli kuwa yeye alikuwa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Basi Raheli alikimbia na kumweleza baba yake. Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani mwake, naye Yakobo akamwambia mambo hayo yote. Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni mwili wangu na damu yangu mwenyewe.”