Mwanzo 27:1-41
Mwanzo 27:1-41 Biblia Habari Njema (BHN)
Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.” Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.” Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina. Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.” Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha. Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.” Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema, “Tazama, harufu nzuri ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu! Mungu akumiminie umande wa mbinguni; akupe ardhi yenye rutuba, nafaka na divai kwa wingi. Jamii za watu zikutumikie, na mataifa yakuinamie kwa heshima. Uwe mtawala wa ndugu zako, watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima. Kila akulaaniye na alaaniwe, kila akubarikiye na abarikiwe!” Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni. Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!” Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.” Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!” Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!” Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.” Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?” Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?” Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa. Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia, “Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba, na mbali na umande wa mbinguni. Utaishi kwa upanga wako, na utamtumikia ndugu yako; lakini utakapoasi utaivunja kongwa yake shingoni mwako.” Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.”
Mwanzo 27:1-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua uta wako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukaniandalie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda mbugani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Nenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si baraka. Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, nenda ukaniletee wana-mbuzi. Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate aliouandaa. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Inuka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau. Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu. Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Alaaniwe yeyote yule atakayekulaani, Na abarikiwe yeyote yule atakayekubariki. Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na punde tu baada ya Yakobo kutoka mbele ya Isaka, babake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake. Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na ainuke, ale mawindo ya mwanawe, ili uweze kunibariki. Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa. Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikuu na chenye uchungu mwingi sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu. Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akaichukua baraka yako. Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa ameichukua baraka yangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka? Isaka akajibu, akamwambia Esau, Tazama, nimemfanya awe bwana wako, na ndugu zake wote nimempa kuwa watumishi wake; kwa nafaka na mvinyo nimemtegemeza, nami nikufanyie nini sasa, mwanangu? Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia. Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia, Angalia, penye manono ya nchi patakuwa makao yako, Na penye umande wa mbingu unaotoka juu. Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo; Na itakuwa utakapoponyoka, Utalivunja kongwa lake katika shingo yako. Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ile baraka babaye aliyombariki. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.
Mwanzo 27:1-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si mbaraka. Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, enenda ukaniletee wana-mbuzi. Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate alioufanya. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau. Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu. Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe. Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na alipokuwa Yakobo ndiyo kwanza ametoka mbele ya Isaka, baba yake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake. Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na aondoke, ale mawindo ya mwanawe, ili roho yako inibariki. Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa. Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu. Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akauchukua mbaraka wako. Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua mbaraka wangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka? Isaka akajibu, akamwambia Esau, Tazama, nimemfanya awe bwana wako, na ndugu zake wote nimempa kuwa watumishi wake; kwa nafaka na mvinyo nimemtegemeza, nami nikufanyie nini sasa, mwanangu? Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia. Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia, Angalia, penye manono ya nchi patakuwa makao yako, Na penye umande wa mbingu unaotoka juu. Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo; Na itakuwa utakapoponyoka, Utalivunja kongwa lake katika shingo yako. Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.
Mwanzo 27:1-41 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.” Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.” Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za BWANA kabla sijafa.’ Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.” Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo. Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.” Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka. Yakobo akaenda kwa baba yake, akasema, “Baba yangu.” Akajibu, “Naam, mwanangu. Wewe ni nani?” Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili unibariki.” Isaka akamuuliza mwanawe, “Umepataje mawindo haraka hivi, mwanangu?” Akajibu, “BWANA Mungu wako amenifanikisha.” Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu, tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.” Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. Akamuuliza, “Kweli wewe ni mwanangu Esau?” Akajibu, “Ni mimi.” Kisha Isaka akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nikubariki.” Yakobo akamletea, naye akala; kisha akamletea na divai akanywa. Ndipo Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.” Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema, “Aha, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba ambalo BWANA amelibariki. Mungu na akupe umande wa mbinguni na utajiri wa duniani: wingi wa nafaka na divai mpya. Mataifa yakutumikie, na mataifa yakusujudie. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie. Walaaniwe wale wanaokulaani, na wabarikiwe wale wanaokubariki.” Baada ya Isaka kumbariki Yakobo, na punde tu alipoondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni. Naye pia akaandaa chakula kitamu, akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.” Isaka baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?” Akamjibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.” Isaka akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!” Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia kwa sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki! Nibariki mimi pia, baba yangu!” Lakini akamjibu, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu, akachukua baraka yako.” Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?” Isaka akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako; pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, na nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?” Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa. Baba yake Isaka akamjibu, “Makao yako yatakuwa mbali na utajiri wa dunia, mbali na umande wa mbinguni. Utaishi kwa upanga, nawe utamtumikia ndugu yako. Lakini utakapokuwa umejikomboa, utatupa nira yake kutoka shingoni mwako.” Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia; ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”