Mwanzo 27:1-10
Mwanzo 27:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.” Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.”
Mwanzo 27:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua uta wako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukaniandalie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda mbugani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Nenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake.
Mwanzo 27:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake.
Mwanzo 27:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.” Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.” Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za BWANA kabla sijafa.’ Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.”