Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 26:12-35

Mwanzo 26:12-35 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki, naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana. Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu. Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.” Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake. Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika, wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye. Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna. Kisha Isaka akaenda mahali pengine na kuchimba kisima kingine. Lakini hicho hawakukigombania; hivyo Isaka akakiita Rehobothi akisema, “Sasa Mwenyezi-Mungu ametuachia nafasi, nasi tutastawi katika nchi hii.” Kutoka huko, Isaka alikwenda Beer-sheba. Usiku huohuo Mwenyezi-Mungu alimtokea na kumwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako Abrahamu. Usiogope kwa kuwa niko pamoja nawe; nitakubariki na kuwazidisha wazawa wako kwa ajili ya Abrahamu, mtumishi wangu.” Kwa hiyo, Isaka akajenga huko madhabahu, akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Akapiga kambi huko; na watumishi wake wakachimba kisima. Abimeleki alitoka Gerari akiwa pamoja na Ahuzathi, mshauri wake, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, akamwendea Isaka. Isaka akawauliza, “Kwa nini mmekuja kwangu hali mnanichukia na mlinifukuza kwenu?” Wao wakamjibu, “Tumeona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe. Kwa hiyo, tunafikiri inafaa tule kiapo pamoja nawe na kufanya agano, kwamba hutatudhuru, nasi kadhalika hatutakudhuru. Tulikutendea mema, tukakuacha uende zako kwa amani, bila kukutendea baya lolote lile. Na sasa wewe ni mbarikiwa wa Mwenyezi-Mungu.” Basi, Isaka akawafanyia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake wakaamka asubuhi na mapema na kula kiapo. Kisha Isaka akawasindikiza na kuagana nao kwa amani. Siku ileile watumishi wa Isaka walimjia na kumpasha habari za kile kisima walichokuwa wamechimba, wakasema, “Tumepata maji!” Basi, Isaka akakiita kisima hicho Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba hata leo. Esau alipokuwa na umri wa miaka arubaini, alioa wake wawili Wahiti: Yudithi bintiye Beeri, na Basemathi bintiye Eloni. Wanawake hao waliyafanya maisha ya Isaka na Rebeka kuwa machungu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 26

Mwanzo 26:12-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mwaka huo Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, naye akapata mavuno mara mia zaidi. BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Abrahamu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza udongo. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu; naye akaviita majina kufuata majina aliyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubariki, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA. Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. Esau alipokuwa mwenye miaka arubaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti. Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.

Shirikisha
Soma Mwanzo 26

Mwanzo 26:12-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng’ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA. Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti. Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.

Shirikisha
Soma Mwanzo 26

Mwanzo 26:12-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, na kwa mwaka huo huo akavuna mara mia, kwa sababu BWANA alimbariki. Isaka akawa tajiri, nayo mali yake ikaendelea kuongezeka hata akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” Basi Isaka akatoka huko, akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya Abrahamu kufa, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa. Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakagundua huko kisima chenye maji safi. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania; akakiita Sitna. Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.” Kutoka pale akaenda Beer-Sheba. Usiku ule BWANA akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Abrahamu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe. Nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.” Isaka akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima. Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake. Isaka akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu, na ninyi mlinichukia na kunifukuza?” Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa BWANA alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu,’ yaani kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe, kwamba hutatudhuru, kama vile nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote, na tukawaaga kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na BWANA.” Basi Isaka akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake asubuhi na mapema wakaapiana. Kisha Isaka akawaruhusu waende zao, wakamwacha kwa amani. Siku hiyo watumishi wa Isaka wakaja, wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!” Naye akakiita Shiba; hadi leo mji huo unaitwa Beer-Sheba. Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti. Hawa walikuwa chanzo cha huzuni kwa Isaka na Rebeka.

Shirikisha
Soma Mwanzo 26