Mwanzo 26:1-34
Mwanzo 26:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti. Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote. Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.” Basi, Isaka akakaa huko Gerari. Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana. Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka. Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.” Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.” Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.” Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki, naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana. Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu. Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.” Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake. Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika, wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye. Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna. Kisha Isaka akaenda mahali pengine na kuchimba kisima kingine. Lakini hicho hawakukigombania; hivyo Isaka akakiita Rehobothi akisema, “Sasa Mwenyezi-Mungu ametuachia nafasi, nasi tutastawi katika nchi hii.” Kutoka huko, Isaka alikwenda Beer-sheba. Usiku huohuo Mwenyezi-Mungu alimtokea na kumwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako Abrahamu. Usiogope kwa kuwa niko pamoja nawe; nitakubariki na kuwazidisha wazawa wako kwa ajili ya Abrahamu, mtumishi wangu.” Kwa hiyo, Isaka akajenga huko madhabahu, akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Akapiga kambi huko; na watumishi wake wakachimba kisima. Abimeleki alitoka Gerari akiwa pamoja na Ahuzathi, mshauri wake, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, akamwendea Isaka. Isaka akawauliza, “Kwa nini mmekuja kwangu hali mnanichukia na mlinifukuza kwenu?” Wao wakamjibu, “Tumeona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe. Kwa hiyo, tunafikiri inafaa tule kiapo pamoja nawe na kufanya agano, kwamba hutatudhuru, nasi kadhalika hatutakudhuru. Tulikutendea mema, tukakuacha uende zako kwa amani, bila kukutendea baya lolote lile. Na sasa wewe ni mbarikiwa wa Mwenyezi-Mungu.” Basi, Isaka akawafanyia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake wakaamka asubuhi na mapema na kula kiapo. Kisha Isaka akawasindikiza na kuagana nao kwa amani. Siku ileile watumishi wa Isaka walimjia na kumpasha habari za kile kisima walichokuwa wamechimba, wakasema, “Tumepata maji!” Basi, Isaka akakiita kisima hicho Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba hata leo. Esau alipokuwa na umri wa miaka arubaini, alioa wake wawili Wahiti: Yudithi bintiye Beeri, na Basemathi bintiye Eloni.
Mwanzo 26:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Abrahamu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Abrahamu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni dada yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anachezacheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni dada yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nilisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa. Mwaka huo Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, naye akapata mavuno mara mia zaidi. BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Abrahamu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza udongo. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu; naye akaviita majina kufuata majina aliyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubariki, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA. Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. Esau alipokuwa mwenye miaka arubaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.
Mwanzo 26:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa. Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng’ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA. Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.
Mwanzo 26:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi njaa kubwa ikatokea katika nchi hiyo, mbali na njaa iliyotokea wakati wa Abrahamu. Isaka akaenda kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari. BWANA akamtokea Isaka, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia. Kaa katika nchi hii kwa kitambo; mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote, na nitatimiza kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako. Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote, na kupitia uzao wako mataifa yote yatabarikiwa, kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, na akatenda yote niliyomwagiza, akahifadhi amri zangu, na hukumu zangu, pamoja na sheria zangu.” Hivyo Isaka akaishi huko Gerari. Wanaume wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Wanaume wa huku wanaweza kuniua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa sura.” Isaka alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake. Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu’?” Isaka akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.” Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotutendea? Ingewezekana mtu yeyote akakutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia kwetu.” Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.” Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, na kwa mwaka huo huo akavuna mara mia, kwa sababu BWANA alimbariki. Isaka akawa tajiri, nayo mali yake ikaendelea kuongezeka hata akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” Basi Isaka akatoka huko, akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya Abrahamu kufa, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa. Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakagundua huko kisima chenye maji safi. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania; akakiita Sitna. Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.” Kutoka pale akaenda Beer-Sheba. Usiku ule BWANA akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Abrahamu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe. Nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.” Isaka akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima. Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake. Isaka akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu, na ninyi mlinichukia na kunifukuza?” Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa BWANA alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu,’ yaani kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe, kwamba hutatudhuru, kama vile nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote, na tukawaaga kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na BWANA.” Basi Isaka akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake asubuhi na mapema wakaapiana. Kisha Isaka akawaruhusu waende zao, wakamwacha kwa amani. Siku hiyo watumishi wa Isaka wakaja, wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!” Naye akakiita Shiba; hadi leo mji huo unaitwa Beer-Sheba. Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti.