Mwanzo 26:1-11
Mwanzo 26:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti. Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote. Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.” Basi, Isaka akakaa huko Gerari. Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana. Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka. Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.” Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.” Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.”
Mwanzo 26:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Abrahamu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Abrahamu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni dada yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anachezacheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni dada yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nilisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.
Mwanzo 26:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.
Mwanzo 26:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi njaa kubwa ikatokea katika nchi hiyo, mbali na njaa iliyotokea wakati wa Abrahamu. Isaka akaenda kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari. BWANA akamtokea Isaka, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia. Kaa katika nchi hii kwa kitambo; mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote, na nitatimiza kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako. Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote, na kupitia uzao wako mataifa yote yatabarikiwa, kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, na akatenda yote niliyomwagiza, akahifadhi amri zangu, na hukumu zangu, pamoja na sheria zangu.” Hivyo Isaka akaishi huko Gerari. Wanaume wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Wanaume wa huku wanaweza kuniua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa sura.” Isaka alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake. Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu’?” Isaka akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.” Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotutendea? Ingewezekana mtu yeyote akakutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia kwetu.” Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”