Mwanzo 24:1-9
Mwanzo 24:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa Abrahamu alikuwa mzee wa miaka mingi, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa amembariki katika kila hali. Siku moja Abrahamu akamwambia mtumishi wake aliyekuwa mzee kuliko wengine na msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako mapajani mwangu, nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao. Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.” Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?” Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko. Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.” Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo.
Mwanzo 24:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na BWANA alikuwa amembariki Abrahamu katika vitu vyote. Abrahamu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali nenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Abrahamu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atamtuma malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Abrahamu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.
Mwanzo 24:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na BWANA alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.
Mwanzo 24:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye BWANA alikuwa amembariki katika mambo yote. Abrahamu akamwambia mtumishi wake mkuu katika nyumba yake, aliyekuwa msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako chini ya paja langu. Ninataka uape kwa BWANA, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao. Bali nenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaka mwanangu mke.” Yule mtumishi akamuuliza, “Je, itakuwaje huyo mwanamke akikataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimrudishe mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?” Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, alinitoa nyumbani mwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa. Ndiye alisema nami na akaniahidi kwa kiapo, akasema, ‘Nitawapa uzao wako nchi hii.’ Yeye atatuma malaika wake akutangulie ili umtwalie mwanangu mke kutoka huko. Huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.” Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu, akamwapia kuhusu shauri hili.