Mwanzo 24:1-51
Mwanzo 24:1-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa Abrahamu alikuwa mzee wa miaka mingi, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa amembariki katika kila hali. Siku moja Abrahamu akamwambia mtumishi wake aliyekuwa mzee kuliko wengine na msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako mapajani mwangu, nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao. Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.” Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?” Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko. Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.” Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo. Kisha, huyo mtumishi akachukua ngamia kumi wa bwana wake akaondoka akiwa na zawadi nzuri za kila aina. Akasafiri kwenda katika mji alimokaa Nahori, nchini Mesopotamia. Alipowasili, aliwapigisha magoti ngamia wake kando ya kisima kilichokuwa nje ya mji. Ilikuwa jioni wakati ambapo wanawake huenda kisimani kuteka maji. Naye akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba unijalie nifaulu leo na umfadhili Abrahamu bwana wangu. Niko hapa kando ya kisima ambapo binti za wenyeji wa mji huja kuteka maji. Basi, msichana nitakayemwambia atue mtungi wake wa maji anipatie maji ninywe, naye akanipa mimi pamoja na kuwanywesha ngamia wangu, na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Jambo hilo litanionesha kwamba umemfadhili bwana wangu.” Kabla hajamaliza kuomba, mara Rebeka, binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu yake Abrahamu, akafika amebeba mtungi wake begani. Msichana huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, na bikira ambaye hakuwa amelala na mwanamume yeyote. Basi, akateremka kisimani, akaujaza mtungi wake maji na kupanda. Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali, nipatie maji ya kunywa kutoka mtungi wako.” Msichana akamjibu, “Haya kunywa bwana wangu.” Na papo hapo akautua mtungi wake, akiushikilia ili amnyweshe. Alipokwisha kumpatia maji, akamwambia, “Nitawatekea maji ngamia wako pia, wanywe mpaka watosheke.” Basi, akafanya haraka, akawamiminia ngamia maji ya mtungi wake katika hori, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na kuwanywesha ngamia wake wote. Yule mtu akawa anamtazama kwa makini bila kusema lolote, apate kufahamu kama Mwenyezi-Mungu ameifanikisha safari yake au sivyo. Ngamia walipotosheka kunywa maji, yule mtu akampa huyo msichana pete ya dhahabu yenye uzito upatao gramu sita, na bangili mbili za dhahabu za gramu kumi kila moja. Akamwuliza, “Niambie tafadhali: Wewe ni binti nani? Je, kuna nafasi ya kulala nyumbani kwenu?” Rebeka akajibu, “Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori. Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha na mahali pa kulala wageni.” Ndipo yule mtu akainamisha kichwa chake, akamwabudu Mwenyezi-Mungu akisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hajasahau fadhili zake na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mwenyezi-Mungu ameniongoza mimi mwenyewe moja kwa moja hadi kwa jamaa ya bwana wangu!” Kisha yule msichana akakimbia kwenda kuwapa habari jamaa za mama yake. Rebeka alikuwa na kaka yake aitwaye Labani. Labani akatoka mbio kukutana na yule mtu kisimani. Labani alikuwa ameiona ile pete na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia mambo Rebeka aliyoambiwa na huyo mtu. Labani alimkuta yule mtu amesimama karibu na ngamia wake kando ya kisima. Labani akamwambia, “Karibu kwetu wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi-Mungu. Mbona unasimama nje? Mimi mwenyewe nimekwisha tayarisha nyumba na mahali kwa ajili ya hawa ngamia wako!” Basi, mtumishi huyo wa Abrahamu akaingia nyumbani. Labani akawafungua ngamia na kuwapatia majani ngamia wake, akampa yeye na watu wake maji ya kunawa miguu. Basi, wakamwandalia chakula, lakini yeye akasema, “Sitakula mpaka nimesema ninachotaka kusema.” Labani akamwambia, “Haya, tuambie.” Yule mtu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. Mwenyezi-Mungu amembariki sana bwana wangu, naye amekuwa mtu maarufu. Amempa makundi ya kondoo na mifugo mingi, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda! Sara, mke wa bwana wangu katika uzee wake, alimzalia bwana wangu mtoto; na bwana wangu amempa huyo mtoto mali yake yote. Bwana wangu aliniapisha mimi akisema, ‘Hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ambao ninaishi katika nchi yao. Bali utakwenda mpaka nchi yangu, kwa jamaa zangu, ili umtafutie mwanangu Isaka mke.’ Nami nikamwambia bwana wangu, ‘Huenda mwanamke huyo akakataa kufuatana nami kuja huku.’ Lakini yeye akasema, ‘Mwenyezi-Mungu aniongozaye maishani mwangu, atamtuma malaika wake aende pamoja nawe na kukufanikisha katika safari yako; nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka kwa jamaa yangu na nyumba ya baba yangu. Kama utakapofika kwa jamaa zangu hawatakupa huyo msichana, basi, hutafungwa na kiapo changu.’ “Leo nilipofika kisimani nimeomba, ‘Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba nifaulu leo katika safari yangu na umfadhili Abrahamu bwana wangu. Niko hapa kando ya kisima. Msichana atakayekuja kuteka maji ambaye nitamwomba anipatie maji kidogo ya kunywa kutoka mtungi wake, naye akanipa na kuwatekea maji ngamia wangu, basi huyo na awe ndiye uliyemchagua kuwa mke wa mwana wa bwana wangu.’ “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, mara Rebeka alifika na mtungi wake wa maji begani, akateremka kisimani na kuteka maji. Nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ya kunywa.’ Naye akautua mtungi wake haraka kutoka begani mwake, akasema, ‘Haya, kunywa bwana wangu. Nitawatekea maji ngamia wako pia.’ Basi mimi nikanywa na ngamia wangu pia akawapa maji. Ndipo nilipomwuliza, ‘Je, wewe ni binti wa nani?’ Akaniambia, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.’ Ndipo nilipompa pete na kumvisha bangili mikononi. Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe. Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.” Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote. Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.”
Mwanzo 24:1-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na BWANA alikuwa amembariki Abrahamu katika vitu vyote. Abrahamu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali nenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Abrahamu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atamtuma malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Abrahamu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Abrahamu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Abrahamu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia wako nitawatekea, hadi watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia wake wote. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kama BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. Yule mtu akainama akamsujudu BWANA. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu. Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa dada yake, akasikia maneno ya Rebeka dada yake, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. Akasema, Mimi ni mtumwa wa Abrahamu, na BWANA amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng'ombe, na fedha, na dhahabu, na watumishi, na wajakazi, na ngamia, na punda. Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo. Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao. Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke. Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami. Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atatuma malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu. Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikia jamaa zangu; hata wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu. Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia wako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe. Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akasema, Unywe, na ngamia wako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao. Kisha nikamwuliza, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia kishaufu puani mwake na vikuku mikononi mwake. Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kulia au wa kushoto. Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa BWANA, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema BWANA.
Mwanzo 24:1-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na BWANA alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. Yule mtu akainama akamsujudu BWANA. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu. Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. Akasema, Mimi ni mtumwa wa Ibrahimu, na BWANA amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng’ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda. Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo. Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao. Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke. Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami. Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu. Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu. Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe. Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao. Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake. Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto. Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa BWANA, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema BWANA.
Mwanzo 24:1-51 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye BWANA alikuwa amembariki katika mambo yote. Abrahamu akamwambia mtumishi wake mkuu katika nyumba yake, aliyekuwa msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako chini ya paja langu. Ninataka uape kwa BWANA, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao. Bali nenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaka mwanangu mke.” Yule mtumishi akamuuliza, “Je, itakuwaje huyo mwanamke akikataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimrudishe mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?” Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, alinitoa nyumbani mwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa. Ndiye alisema nami na akaniahidi kwa kiapo, akasema, ‘Nitawapa uzao wako nchi hii.’ Yeye atatuma malaika wake akutangulie ili umtwalie mwanangu mke kutoka huko. Huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.” Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu, akamwapia kuhusu shauri hili. Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia wa bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Mesopotamia, akaenda hadi mji wa Nahori. Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji; ilikuwa inaelekea jioni, wakati wanawake huteka maji. Kisha akaomba, “Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nipatie ushindi leo, uoneshe ukarimu kwa bwana wangu Abrahamu. Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji. Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmoja, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji’; naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia’: basi na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Kwa hili nitajua umemtendea bwana wangu ukarimu.” Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka, aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu. Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mwanaume aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake, tena akapanda juu. Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.” Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa. Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitawatekea ngamia wako maji pia hadi wote watosheke.” Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine, na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote. Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama BWANA ameifanikisha safari yake, au la. Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja, na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi. Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti ya nani? Tafadhali niambie. Je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tunapoweza kulala?” Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.” Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.” Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu BWANA, akisema, “Atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, BWANA ameniongoza safarini, akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.” Yule msichana akakimbia, akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya. Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani; huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani. Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima. Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na BWANA. Kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.” Hivyo yule mtumishi akaingia nyumbani, nayo mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia, na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu. Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula hadi niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.” Labani akasema, “Basi tuambie.” Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. BWANA amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho. Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao, ila uende hadi kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’ “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’ “Akanijibu, ‘BWANA, ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu. Kisha, utakapoenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu. Hata wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’ “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia. Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki. Mwanamwali akija kuteka maji, nami nikimwambia: Tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka mtungi wako. Naye akiniambia, “Kunywa, nami nitawatekea ngamia wako maji pia,” basi huyo awe ndiye mke BWANA amemchagulia mwana wa bwana wangu.’ “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani, akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’ “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa, na nitawanywesha ngamia wako pia.’ Basi nikanywa, naye akawanywesha na ngamia pia. “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti ya nani?’ “Akasema, ‘Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’ “Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake, nikasujudu na nikamwabudu BWANA. Nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake. Ikiwa mtaonesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie; la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.” Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa BWANA; hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema. Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na BWANA alivyoongoza.”