Mwanzo 22:6-14
Mwanzo 22:6-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja. Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?” Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao. Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu. Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!” Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.” Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.”
Mwanzo 22:6-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Abrahamu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Abrahamu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Abrahamu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Abrahamu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Abrahamu! Abrahamu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, kwa kuwa hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Abrahamu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo dume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Abrahamu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Abrahamu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.
Mwanzo 22:6-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.
Mwanzo 22:6-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Abrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, naye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, Isaka akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!” Abrahamu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.” Isaka akasema, “Moto na kuni zipo. Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?” Abrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja. Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. Lakini malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!” Akajibu, “Mimi hapa.” Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.” Abrahamu akainua macho, akaona nyuma yake kondoo dume akiwa amenaswa pembe zake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Abrahamu akapaita mahali pale Yehova-Yire. Hadi leo inasemekana, “Katika mlima wa BWANA itapatikana.”