Mwanzo 22:3-10
Mwanzo 22:3-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu. Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali. Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.” Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja. Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?” Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao. Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu. Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe.
Mwanzo 22:3-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Abrahamu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Abrahamu akainua macho yake, akapaona mahali pakiwa bado ni mbali. Abrahamu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. Basi Abrahamu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Abrahamu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Abrahamu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Abrahamu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
Mwanzo 22:3-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
Mwanzo 22:3-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Abrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. Siku ya tatu Abrahamu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunaenda kule. Tutaabudu na kisha tutawarudia.” Abrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, naye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, Isaka akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!” Abrahamu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.” Isaka akasema, “Moto na kuni zipo. Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?” Abrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja. Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.