Mwanzo 21:1-34
Mwanzo 21:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!” Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa. Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.” Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba. Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti. Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake. Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri. Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.” Abrahamu akasema, “Naapa.” Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya. Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.” Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao. Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba. Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?” Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.” Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo. Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti. Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele. Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu.
Mwanzo 21:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Abrahamu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akamtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yalipoisha katika kiriba, Hajiri akamlaza kijana kichakani. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri. Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Abrahamu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda. Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake. Abrahamu akasema, Nitaapa. Kisha Abrahamu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki wamemnyang'anya. Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu. Abrahamu akatwaa kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano. Abrahamu akawaweka wana-kondoo saba wa kike peke yao. Abimeleki akamwuliza Abrahamu, Hawa wana-kondoo saba majike, uliowaweka, maana yake ni nini? Akasema, Hawa wana-kondoo saba majike utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki. Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili. Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti. Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la BWANA Mungu wa milele. Abrahamu akaishi kama mgeni kwa Wafilisti siku nyingi.
Mwanzo 21:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri. Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda. Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake. Ibrahimu akasema, Nitaapa. Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang’anya. Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu. Ibrahimu akatwaa kondoo na ng’ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano. Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao. Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini? Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki. Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili. Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti. Ibrahimu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la BWANA Mungu wa milele. Ibrahimu akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.
Mwanzo 21:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huu BWANA akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na BWANA akamtendea Sara kama alivyoahidi. Sara akapata mimba, na akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi. Abrahamu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa. Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.” Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa. Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki. Hivyo Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe. Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.” Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hajiri. Akaviweka begani mwa Hajiri, akamwondoa pamoja na kijana. Hajiri akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba. Maji yalipokwisha kwenye kiriba, Hajiri akamwacha kijana chini ya kichaka. Kisha akaenda akaketi kama umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Akiwa ameketi pale, akaanza kulia kwa huzuni. Mungu akamsikia kijana akilia. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini, Hajiri? Usiogope, Mungu amesikia kijana akilia akiwa amelala pale. Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.” Ndipo Mungu akamfumbua Hajiri macho, akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe. Mungu akawa pamoja na huyo kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde. Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akamtwalia mke kutoka Misri. Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.” Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.” Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyangʼanya. Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.” Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. Abrahamu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi. Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?” Abrahamu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.” Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo. Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti. Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la BWANA, Mungu wa milele. Naye Abrahamu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.