Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 2:1-25

Mwanzo 2:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa. Siku ile Mwenyezi-Mungu alipoziumba mbingu na dunia, Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima. Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote. Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai. Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba. Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne. Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu. Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu. Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi. Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate. Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani; lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile, maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao. Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa. Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama. Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume. Ndipo huyo mwanamume akasema, “Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu, na nyama kutoka nyama yangu. Huyu ataitwa ‘Mwanamke’, kwa sababu ametolewa katika mwanamume.” Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja. Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya.

Shirikisha
Soma Mwanzo 2

Mwanzo 2:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi mbingu na nchi zikamalizika kuumbwa, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilivyoumbwa. Siku ile BWANA Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana BWANA Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; maji yakapanda katika nchi, yakatia unyevu juu ya uso wote wa ardhi. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa kiumbe hai. BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne. Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham. Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati. BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, “Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, Lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. BWANA Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.

Shirikisha
Soma Mwanzo 2

Mwanzo 2:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile BWANA Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana BWANA Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne. Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham. Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati. BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. BWANA Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.

Shirikisha
Soma Mwanzo 2

Mwanzo 2:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo. Kufikia siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya; hivyo siku hiyo ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. Mungu akaibariki siku ya saba, akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika baada ya kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya. Haya ndio maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa. BWANA Mungu alipoziumba mbingu na dunia, hapakuwa na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwa na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa BWANA Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwa na mtu wa kuilima ardhi, lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi. BWANA Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai. Basi BWANA Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni; huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. BWANA Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Mti wa uzima ulikuwa katikati ya bustani, na pia mti wa kujua mema na mabaya. Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni; kuanzia hapo ukagawanyika kuwa mito minne. Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri; bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati. BWANA Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani; lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.” BWANA Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” Basi BWANA Mungu alikuwa ametengeneza kutoka ardhi wanyama pori wote, na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa jina lake. Hivyo Adamu akawapa majina mifugo wote, ndege wa angani, na wanyama pori wote. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. Hivyo BWANA Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. Kisha BWANA Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwa ule ubavu alioutoa kwa mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa mwanaume. Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke’, kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.” Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Adamu na mkewe wote walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 2

Mwanzo 2:1-25

Mwanzo 2:1-25 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima