Mwanzo 17:1-8
Mwanzo 17:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi-Mungu alimtokea, akamwambia, “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama. Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.” Hapo Abramu akasujudu. Naye Mungu akamwambia, “Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba wa mataifa mengi. Tangu sasa, hutaitwa tena Abramu, bali utaitwa Abrahamu, maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana; kwako nitazusha mataifa mengi na wafalme. Nitalithibitisha agano langu nawe, wazawa wako na vizazi vyao vyote milele; tena nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako milele. Nitakupa wewe na wazawa wako nchi hii ambamo unaishi kama mgeni; yaani nchi yote ya Kanaani iwe mali yenu milele; nami nitakuwa Mungu wao.”
Mwanzo 17:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na tisa, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu nawe, nami nitakuzidishia sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, Hili ndilo agano langu nawe, utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Abrahamu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati yangu na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayokaa kama mgeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.
Mwanzo 17:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.
Mwanzo 17:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, BWANA akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; nenda mbele zangu na uishi kwa unyofu. Nitafanya agano kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana.” Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, “Kwangu mimi, hili ndilo agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. Hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana; kwako yatatoka mataifa, na wafalme watatoka kwako. Nitalithibitisha agano langu kama agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo, nami nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazao wako. Nchi yote ya Kanaani, unayoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na ya uzao wako; nami nitakuwa Mungu wao.”