Mwanzo 16:1-3
Mwanzo 16:1-3 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Sarai, mkewe Abramu, alikuwa bado hajamzalia mumewe mtoto. Lakini alikuwa na mjakazi aliyeitwa Hagari, kutoka Misri. Basi, Sarai akamwambia Abramu, “Unajua kuwa Mwenyezi-Mungu hajanijalia kupata watoto. Mchukue Hagari mjakazi wangu; huenda nikapata watoto kwake.” Abramu akakubali shauri la Sarai. Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mjakazi wake ambaye alikuwa Mmisri, awe mke wake. Haya yalitokea baada ya Abramu kukaa katika nchi ya Kanaani kwa muda wa miaka kumi.
Mwanzo 16:1-3 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, kwa kuwa BWANA amenifunga tumbo nisizae, sasa mwingilie mjakazi wangu, labda nitapata uzao kutoka kwake. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Kwa hiyo, baada ya Abramu kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani, Sarai mkewe Abramu alimtwaa Hajiri Mmisri, mjakazi wake, akampa Abramu mumewe, kama mke.
Mwanzo 16:1-3 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe.
Mwanzo 16:1-3 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mjakazi Mmisri jina lake Hajiri. Hivyo Sarai akamwambia Abramu, “BWANA amenizuilia kupata watoto. Basi nenda ukutane kimwili na mjakazi wangu; huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.” Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mjakazi wake Mmisri aliyeitwa Hajiri, na kumpa mumewe awe mke wake.