Mwanzo 13:1-18
Mwanzo 13:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu. Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai, ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema. Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja. Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja. Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.” Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora). Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana. Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu. Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele. Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika! Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.” Kwa hiyo, Abramu akangoa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre kule Hebroni; huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu.
Mwanzo 13:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza, kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu jamaa moja. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi jitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kulia; ukienda upande wa kulia, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma. Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA. BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele. Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; ikiwa mtu ataweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika. Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo. Basi Abramu akahamisha hema yake, akaja na kukaa karibu na mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.
Mwanzo 13:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma. Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA. BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele. Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika. Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo. Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.
Mwanzo 13:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho; pia Lutu akaenda pamoja naye. Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu. Kutoka Negebu, akasafiri sehemu mbalimbali hadi akafika Betheli, mahali ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai, pale alipokuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la BWANA. Basi Lutu, aliyekuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na mifugo na mahema. Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali yao. Ukazuka ugomvi kati ya wafugaji wa wanyama wa Abramu na wale wa Lutu. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi pia waliishi katika nchi hiyo. Hivyo Abramu akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Ukielekea kushoto, nitaenda kulia; ukielekea kulia, mimi nitaenda kushoto.” Lutu akatazama, akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora.) Hivyo Lutu akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana. Abramu aliishi nchi ya Kanaani, naye Lutu akaishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma. Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakitenda dhambi nyingi dhidi ya BWANA. Baada ya Lutu kuondoka, BWANA akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi. Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele. Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo ikiwa kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika. Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.” Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni. Naye akamjengea BWANA madhabahu huko.