Mwanzo 13:1-11
Mwanzo 13:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu. Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai, ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema. Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja. Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja. Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.” Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora). Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana.
Mwanzo 13:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza, kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu jamaa moja. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi jitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kulia; ukienda upande wa kulia, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.
Mwanzo 13:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.
Mwanzo 13:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho; pia Lutu akaenda pamoja naye. Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu. Kutoka Negebu, akasafiri sehemu mbalimbali hadi akafika Betheli, mahali ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai, pale alipokuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la BWANA. Basi Lutu, aliyekuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na mifugo na mahema. Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali yao. Ukazuka ugomvi kati ya wafugaji wa wanyama wa Abramu na wale wa Lutu. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi pia waliishi katika nchi hiyo. Hivyo Abramu akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Ukielekea kushoto, nitaenda kulia; ukielekea kulia, mimi nitaenda kushoto.” Lutu akatazama, akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora.) Hivyo Lutu akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana.