Mwanzo 12:1-7
Mwanzo 12:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka. Anayekubariki, nitambariki; anayekulaani, nitamlaani. Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.” Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru; na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani. Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani, Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu, mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea.
Mwanzo 12:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani. Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye akamjengea BWANA madhabahu huko alikomtokea.
Mwanzo 12:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani. Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea.
Mwanzo 12:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA alikuwa amemwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha. “Nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki, Nitalikuza jina lako, nawe utakuwa baraka. Nitawabariki wale wanaokubariki, na yeyote akulaaniye nitamlaani; na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.” Hivyo Abramu akaondoka kama BWANA alivyokuwa amemwambia; naye Lutu akaondoka pamoja naye. Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na umri wa miaka sabini na tano. Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake, mali yote waliyokuwa nayo, pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri kwenda nchi ya Kanaani, na wakafika huko. Abramu akasafiri katika nchi hiyo hadi huko Shekemu, mahali penye mwaloni wa More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo. BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapo akamjengea madhabahu BWANA aliyekuwa amemtokea.