Mwanzo 1:1-12
Mwanzo 1:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji. Mungu akasema, “Mwanga uwe.” Mwanga ukawa. Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza, mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza. Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo. Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo. Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
Mwanzo 1:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa tupu, tena bila umbo, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akaliumba anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mimea itoayo mbegu, na miti ya matunda izaayo matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
Mwanzo 1:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
Mwanzo 1:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji. Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema; ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. Mungu akaiita nuru “mchana”, na giza akaliita “usiku”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji, igawe maji na maji.” Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. Mungu akaiita hiyo nafasi “anga”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. Mungu akaiita nchi kavu “ardhi”, nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema.