Wagalatia 6:7-18
Wagalatia 6:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu. Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: Kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli – watu wa Mungu. Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina.
Wagalatia 6:7-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. Tazameni niandikavyo kwa herufi kubwa niwaandikiapo kwa mkono wangu mimi mwenyewe! Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. Lakini mimi, la hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutotahiriwa, ila kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
Wagalatia 6:7-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe! Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
Wagalatia 6:7-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waumini. Angalieni herufi kubwa ninazotumia nikiwaandikia kwa mkono wangu mwenyewe! Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo. Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. Lakini mimi naomba nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwake ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, hata kwa Israeli wa Mungu. Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.