Wagalatia 4:8-31
Wagalatia 4:8-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mliitumikia miungu isiyo miungu kweli. Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena? Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka! Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure! Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama nyinyi. Hamkunitendea ubaya wowote. Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Injili kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe. Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyangoa macho yenu na kunipa mimi. Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli? Hao watu wengine wanawahangaikia nyinyi, lakini nia yao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili nyinyi muwahangaikie wao. Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi. Watoto wangu, kama vile mama mjamzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu. Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi! Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo sheria? Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: Mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru. Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani. Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake. Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu. Maana imeandikwa: “Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi kuliko wa yule aliye na mume.” Sasa, basi, ndugu zangu, nyinyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka. Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi. Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: “Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru.” Hivyo basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.
Wagalatia 4:8-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu. Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lolote. Lakini mwajua ya kuwa niliwahubiria Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. Kuko wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi. Je! Nimekuwa adui yenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli? Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa nia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku. Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu. Watoto wangu wadogo, ambao nawaonea uchungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu; laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu. Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria? Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Abrahamu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mwingine kwa mwanamke huru. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwanamke huru kwa ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa yuko utumwani pamoja na watoto wake. Bali Yerusalemu wa juu ni muungwana, naye ndiye mama yetu sisi. Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na uchungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume. Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa muungwana. Kwa hiyo, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye muungwana.
Wagalatia 4:8-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu. Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lo lote. Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling’oa macho yenu, mkanipa mimi. Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli? Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa njia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku. Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu. Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu; laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu. Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria? Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto. Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi. Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume. Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.
Wagalatia 4:8-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure. Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya. Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili. Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu. Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imeenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngengʼoa macho yenu na kunipa mimi. Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia ukweli? Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku. Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu. Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea uchungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu. Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu. Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema? Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru. Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, linalozaa watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hajiri. Basi Hajiri anawakilisha Mlima Sinai ulio Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake. Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu. Kwa maana imeandikwa: “Furahi, ewe mwanamke tasa, wewe usiyezaa; paza sauti, na kuimba kwa furaha, wewe usiyepatwa na uchungu wa kuzaa; kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume.” Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaka, tu watoto wa ahadi. Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa. Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.” Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.