Wagalatia 4:1-11
Wagalatia 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nasema hivi: Mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake. Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake. Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu. Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu. Kwa vile sasa nyinyi ni wanawe, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia “Aba,” yaani “Baba.” Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake. Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mliitumikia miungu isiyo miungu kweli. Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena? Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka! Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!
Wagalatia 4:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ni bwana wa yote; bali yuko chini ya mawakili na watunzaji, hadi wakati uliokwisha kuamriwa na baba. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia. Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu. Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.
Wagalatia 4:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu. Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.
Wagalatia 4:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. Yeye huwa chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini hadi ufike wakati uliowekwa na baba yake. Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu. Lakini wakati uliopangwa ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria, ili awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, nasi tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa wana. Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.” Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mwana. Na kwa kuwa wewe ni mwana, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kupitia kwa Kristo. Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.