Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 2:1-10

Wagalatia 2:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami. Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Injili niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa, isije ikawa bure. Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa, ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa. Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima. Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi – kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje – watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea. Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi. Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine. Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi. Wakatuomba lakini kitu kimoja: Tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.

Wagalatia 2:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha, baada ya miaka kumi na nne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu, wakati huu pamoja na Barnaba, na nikamchukua Tito pia. Nilienda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. Lakini hata Tito aliyekuwa nami, na alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani, hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili ukweli wa Injili ubaki nanyi. Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote. Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. Basi Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupatia mkono wa shirika, mimi na Barnaba, walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa, na wao waende kwa Wayahudi. Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.