Wagalatia 1:11-16
Wagalatia 1:11-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu. Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia. Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa. Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu. Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie. Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanawe kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu
Wagalatia 1:11-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana, ndugu zangu, Injili hiyo niliyowahubiria, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami niliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubirie Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu
Wagalatia 1:11-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu
Wagalatia 1:11-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo. Ninyi mmekwisha kusikia kuhusu maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika langu, maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote