Ezra 1:5-11
Ezra 1:5-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, wakaondoka viongozi wa koo za makabila ya Yuda na Benyamini, makuhani na Walawi, na kila mtu ambaye Mungu alimpa moyo wa kwenda kujenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, iliyoko Yerusalemu. Majirani waliwasaidia watu hao kwa kuwapa vyombo vya fedha, dhahabu, mali, wanyama na vitu vingine vya thamani, mbali na vile vilivyotolewa kwa hiari. Mfalme Koreshi aliwarudishia vyombo ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuviweka katika nyumba ya miungu yake. Alimkabidhi Mithredathi, mtunza hazina, vyombo hivyo, naye akamhesabia Sheshbaza, mtawala wa Yuda. Ifuatayo ndiyo hesabu yake: Bakuli 30 za dhahabu; bakuli 1,000 za fedha; vyetezo 29; bakuli ndogo za dhahabu 30; bakuli ndogo za fedha 410; vyombo vinginevyo 1,000. Vyombo vyote vya dhahabu na fedha, pamoja na vitu vinginevyo vilikuwa jumla yake 5,400. Vyote hivi, Sheshbaza alivichukua hadi Yerusalemu wakati yeye pamoja na watu wengine alipotolewa uhamishoni Babuloni kwenda Yerusalemu.
Ezra 1:5-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo wakaondoka wakuu wa koo za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu ameamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya BWANA, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu. Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadneza toka Yerusalemu, na kuvitia katika nyumba ya miungu yake. Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda. Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu moja, visu ishirini na tisa; mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu moja. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.
Ezra 1:5-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya BWANA, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu. Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu, na kuvitia katika nyumba ya miungu yake. Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda. Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu, visu ishirini na kenda; mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.
Ezra 1:5-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha viongozi wa jamaa ya Yuda na Benyamini na makuhani na Walawi kila mmoja ambaye moyo wake ulisukumwa na Mungu, akajiandaa kupanda ili kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu. Majirani zao wote wakawasaidia vyombo vya fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, pia na zawadi za thamani, pamoja na sadaka zote za hiari. Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la BWANA, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake. Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda. Hii ilikuwa orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa thelathini; masinia ya fedha yalikuwa elfu moja; vyetezo vya fedha vilikuwa ishirini na tisa; mabakuli ya dhahabu yalikuwa thelathini; mabakuli ya fedha yaliyofanana yalikuwa mia nne na kumi; vifaa vingine vilikuwa elfu moja. Kwa jumla, kulikuwa na vyombo elfu tano na mia nne vya dhahabu na vya fedha.