Ezra 1:1-4
Ezra 1:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia litimie, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake na kuiweka katika maandishi: “Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni na ameniagiza nimjengee nyumba Yerusalemu, huko Yuda. Basi sasa, kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake, Mungu wake awe naye na aende Yerusalemu huko Yuda, na kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, Mungu anayeabudiwa huko Yerusalemu. Kila mmoja aliyebaki hai uhamishoni akitaka kurudi, jirani zake na wamsaidie kwa kumpa fedha, dhahabu, mali na wanyama, pamoja na matoleo ya hiari kwa ajili ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu.”
Ezra 1:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akaamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya BWANA, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu yeyote aliyesalia mahali popote akaapo kama mgeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu.
Ezra 1:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya BWANA, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu.
Ezra 1:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la BWANA lililosemwa na nabii Yeremia, BWANA aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi: “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “ ‘BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. Yeyote kati ya watu wa Mungu miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la BWANA, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko Yerusalemu. Nao wakazi wa popote manusura wanapoishi sasa, wawape manusura fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’ ”