Ezekieli 30:20-26
Ezekieli 30:20-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya saba ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Nimeuvunja mkono wa Farao mfalme wa Misri, nao haukufungwa ili uweze kupona na kuweza kushika upanga. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana na Farao mfalme wa Misri. Nitaivunja mikono yake yote miwili, ule mzima na hata uliovunjika. Na upanga ulio mkononi mwake utaanguka chini. Nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa na kuwasambaza katika nchi nyingine. Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaitia nguvu na kutia upanga wangu mkononi mwake. Lakini nitaivunja mikono ya Farao, naye atapiga kite mbele ya mfalme wa Babuloni kama mtu aliyejeruhiwa vibaya sana. Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaiimarisha, lakini mikono ya Farao italegea. Hapo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakapotia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babuloni, ataunyosha dhidi ya nchi ya Misri, nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Ezekieli 30:20-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha upanga ulio katika mkono wake. Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali. Nami nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, na kuutia upanga wangu katika mkono wake, bali mikono ya Farao nitaivunja, naye ataugua mbele yake, kwa mauguzi ya mtu aliyetiwa jeraha la kumwua. Nami nitaitegemeza mikono ya mfalme wa Babeli, na mikono ya Farao itaanguka; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoutia upanga wangu katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye ataunyosha juu ya nchi ya Misri. Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 30:20-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha upanga ulio katika mkono wake. Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali. Nami nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, na kuutia upanga wangu katika mkono wake, bali mikono ya Farao nitaivunja, naye ataugua mbele yake, kwa mauguzi ya mtu aliyetiwa jeraha ya kumfisha. Nami nitaitegemeza mikono ya mfalme wa Babeli, na mikono ya Farao itaanguka; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoutia upanga wangu katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye ataunyosha juu ya nchi ya Misri. Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 30:20-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga. Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake. Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi zote. Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha. Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri. Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.”