Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 29:1-14

Ezekieli 29:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mgeukie Farao mfalme wa Misri, utoe unabii juu yake na nchi yote ya Misri. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana na wewe mfalme wa Misri, wewe mamba ulalaye mtoni Nili! Wewe unafikiri kwamba Nili ni wako, kwamba wewe ndiwe uliyeufanya! Basi, nitakutia ndoana tayani mwako, na kufanya samaki wakwame magambani mwako. Nitakuvua kutoka huko mtoni. Nitakutupa jangwani, wewe na samaki hao wote. Mwili wako utaanguka mbugani; wala hakuna atakayekuokota akuzike. Nimeutoa mwili wako uwe chakula cha wanyama wakali na ndege. Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete. Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazusha upanga dhidi yako na kuwaua watu na wanyama wako wote. Kwa sababu umesema kuwa mto Nili ni wako, kwamba ndiwe uliyeufanya, basi, nchi yako, Misri, itakuwa tupu na jangwa. Ndipo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Hakika nitakuadhibu wewe na mito yako; kwa hiyo nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na tupu toka Migdoli mpaka Syene hadi mipakani mwa Kushi. Hakuna mtu wala mnyama atakayepita huko. Haitakaliwa kwa muda wa miaka arubaini. Kati ya miji yote iliyoharibiwa, miji ya Misri itakuwa mitupu kwa miaka arubaini. Nitawatawanya Wamisri kati ya watu wa mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine. “Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka arubaini nitawakusanya Wamisri kutoka kwa mataifa walimotawanywa. Nitawafanikisha tena Wamisri. Nitawarudisha katika nchi ya Pathrosi, nchi yao ya asili. Huko watakuwa na ufalme usio na nguvu

Ezekieli 29:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote; nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu. Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako. Nami nitakuacha ukiwa umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka katika uwanda ulio wazi; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani. Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli. Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote. Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama. Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya. Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi. Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arubaini. Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arubaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arubaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hayo makabila ya watu, ambazo walitawanyika kati yao; nami nitawarejesha Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha Pathrosi, nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.

Ezekieli 29:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote; nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu. Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako. Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani. Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli. Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote. Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama. Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya. Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi. Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini. Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao; nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.

Ezekieli 29:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote. Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri, ewe mnyama mkubwa ulalaye katikati ya vijito vyako. Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe; niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.” Lakini nitatia ndoana katika mataya yako nami nitawafanya samaki wa vijito vyako washikamane na magamba yako. Nitakutoa katikati ya vijito vyako, pamoja na samaki wote walioshikamana na magamba yako. Nitakutupa jangwani, wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako. Utaanguka uwanjani, nawe hutakusanywa au kuchukuliwa. Nitakutoa uwe chakula kwa wanyama wa nchi na ndege wa angani. Ndipo wale wote wanaoishi Misri watajua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli. Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka. “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao. Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliuumba,” kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpaka wa Kushi. Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini. Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine. “ ‘Lakini hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa. Nitawarejesha hao Wamisri kutoka kutekwa kwao na kuwaweka Pathrosi, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu.