Ezekieli 21:1-31
Ezekieli 21:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani. “Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Upanga! Naam, upanga umenolewa, nao umengarishwa pia. Umenolewa ili ufanye mauaji, umengarishwa umetamete kama umeme! Umenolewa na kungarishwa uwekwe mkononi mwa mwuaji. Wewe mtu, lia na kuomboleza upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu, dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu. Jipige kifua kwa huzuni. Hilo litakuwa jaribio gumu sana. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe mtu, tabiri! Piga makofi, upanga na ufanye kazi yake, mara mbili, mara tatu. Huo ni upanga wa mauaji nao unawazunguka. Kwa hiyo wamekufa moyo na wengi wanaanguka. Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote. Umefanywa ungae kama umeme, umengarishwa kwa ajili ya mauaji. Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto; elekeza ncha yako pande zote. Nami nitapiga makofi, nitatosheleza ghadhabu yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Chora njia mbili ambapo utapitia upanga wa mfalme wa Babuloni. Njia zote mbili zianzie katika nchi moja. Mwanzoni mwa kila njia utaweka alama ya kuonesha upande mji uliko. Utachora njia upanga utakapopitia kwenda kuufikilia mji wa Raba wa Waamoni, na njia nyingine inayoelekea mji wenye ngome wa Yerusalemu nchini Yuda. Mfalme wa Babuloni anasimama mwanzoni mwa hizo njia mbili, kwenye njia panda, apate kupiga bao. Anatikisa mishale, anaviuliza shauri vinyago vya miungu yake na kuchunguza maini ya mnyama. Mshale unaodokezea ‘Yerusalemu’ umeangukia mkono wake wa kulia. Anaweka zana za kubomolea, anaamuru mauaji na kelele za vita zifanywe, zana za kubomolea malango zimewekwa, maboma na minara ya kuuzingira mji vimewekwa. Lakini watu wa Yerusalemu wataudhania kuwa ni utabiri wa uongo kwa sababu wamekula kiapo rasmi. Hata hivyo unabii huu utawakumbusha uovu wao na kusababishwa kukamatwa kwao. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wataweza kuziona dhambi zenu. Kila mtu atajua jinsi mlivyo na hatia. Kila kitendo mnachotenda kinaonesha dhambi zenu. Nyinyi mmehukumiwa adhabu nami nitawatia mikononi mwa maadui zenu. “Nawe mtawala wa Israeli wewe ni mpotovu kabisa. Siku yako imefika, naam, siku ya adhabu yako ya mwisho. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi: Vua kilemba chako na taji yako kwani mambo hayatabaki kama yalivyokuwa. Walio chini watakwezwa, walio juu watashushwa! Uharibifu! Uharibifu! Hamna chochote katika mji huu nitakachosaza. Lakini kabla ya hayo atakuja yule ambaye nimempa mamlaka ya kuuadhibu, ambaye mimi nitampa mji huo. “Ewe mtu, tabiri kuhusu Waamoni na maneno yao ya dhihaka kwa Waisraeli: Waambie kuwa nasema: Upanga, upanga! Upanga umenyoshwa kuua, umenolewa uangamize, umengarishwa ungae kama umeme. Wakati nyinyi mmetulia katika maono yenu madanganyifu na utabiri wenu wa uongo, upanga utakuwa tayari kukata shingo za waasi na waovu. Siku imewadia ambapo maovu yenu yataadhibiwa. “Sasa rudisha upanga alani mwake! Nitawahukumu mahali palepale mlipoumbwa, katika nchi mlipozaliwa. Nitawamwagia ghadhabu yangu. Moto wa ghadhabu yangu nitaupuliza juu yenu. Nitawatia mikononi mwa watu wakatili, watu hodari wa kuangamiza.
Ezekieli 21:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mwovu, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hadi kaskazini, na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. Piga kite, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika moyo na uchungu mwingi mbele ya macho yao. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unapiga kite? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatageuka kuwa kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. Nao umetolewa ili ung'arishwe upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. Jiweke tayari, nenda upande wa kulia; jipange, nenda upande wa kushoto; mahali popote utakapouelekeza uso wako. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili. Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utachora njia, ili upanga upate kufikia Raba wa wana wa Amoni, na kufikia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huku na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, livue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, kuhusu wana wa Amoni, na kuhusu aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umeng'arishwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; wakati wanapokupa maono ya udanganyifu, wakati wanapokuagulia uongo, wanakuweka juu ya shingo zao wachukizao, na waovu, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa adhabu ya mwisho. Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza.
Ezekieli 21:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kuelekea Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini, na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili. Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari za wana wa Amoni, na katika habari za aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umesuguliwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; wakati wakuoneapo ubatili, wakati wakufanyiao uganga wa uongo, ili kukuweka juu ya shingo zao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho. Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza.
Ezekieli 21:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli uiambie: ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu. Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utatolewa alani mwake uwe dhidi ya kila mtu kuanzia kusini hadi kaskazini. Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi BWANA nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’ “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi. Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatendeka, asema BWANA Mwenyezi.” Neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: “ ‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa: umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ungʼae kama miali ya radi! “ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unadharau kila fimbo kama hiyo. “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji. Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako. “ ‘Lazima kuwe na kujaribiwa. Itakuwaje basi ikiwa fimbo ya ufalme ya Yuda inayodharauliwa na upanga haitakuwepo tena? asema BWANA Mwenyezi.’ “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa mauaji, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande. Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa mauaji kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama miali ya radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua. Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa. Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi BWANA nimesema.” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini. Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome. Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama. Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka magogo ya kubomoa, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka magogo ya kubomoa dhidi ya malango, kupandisha kilima hadi kuta zako, na kujenga husuru dhidi yako. Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha kuhusu uovu wao na kuwachukua mateka. “Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: ‘Kwa sababu ninyi mmefanya uovu wenu ukumbukwe kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mnayoyafanya: kwa kuwa mmefanya hivi, mtachukuliwa mateka. “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yake imewadia, ambaye wakati wake wa adhabu umefikia kilele chake; hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa vile yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa, na aliyekwezwa atashushwa. Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya hadi aje yule aliye mwenye taji kwa haki; huyo ndiye nitakayempa.’ “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi kuhusu Waamoni na matukano yao: “ ‘Upanga, upanga, umefutwa kwa ajili ya kuua, umesuguliwa ili kuangamiza na unametameta kama miali ya radi! Wakati wanatoa maono ya uongo juu yako, na wanapobashiri uongo juu yako, upanga utawekwa kwenye shingo za wapotovu watakaouawa, wale siku yao imewadia, wakati wa adhabu yao ya mwisho. “ ‘Urudishe upanga kwenye ala yake! Katika mahali ulipoumbiwa, katika nchi ya baba zako, huko nitakuhukumu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako; nitakutia mikononi mwa watu wakatili, watu stadi katika kuangamiza.