Ezekieli 20:1-49
Ezekieli 20:1-49 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwaka wa saba tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa tano, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja kumwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, wakaketi mbele yangu. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, sema na hao wazee wa Israeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Je, mmekuja kuniuliza shauri? Hakika, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kuwa sitakubali kuulizwa kitu na nyinyi. “Wewe mtu, je, uko tayari kuwahukumu watu hawa? Basi, wahukumu. Wajulishe waliyofanya wazee wao. Waambie kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nilipowachagua Waisraeli niliwaapia wazawa wa Yakobo. Nilijidhihirisha kwao nchini Misri, nikawaapia nikisema: Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Niliwaambia: ‘Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda; msijitie unajisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.’ Lakini waliniasi, hawakutaka kunisikiliza. Hakuna hata mmoja wao aliyetupilia mbali machukizo yale waliyoyapenda, wala hawakuachana na sanamu za miungu ya Misri. Basi, nikafikiri kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao wakiwa kulekule nchini Misri. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa heshima ya jina langu ili lisidharauliwe kati ya watu wa mataifa wanaoishi nao, hao walioona nikijijulisha kwa Waisraeli wakati wa kuwatoa katika nchi ya Misri. “Basi, mimi niliwatoa nchini Misri, nikawapeleka jangwani. Niliwapa kanuni zangu na kuwafundisha amri zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Niliwapa pia Sabato zangu ziwe ishara kati yangu na wao, wapate kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. Lakini Waisraeli waliniasi huko jangwani; hawakuzifuata kanuni zangu, bali walizikataa sheria zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Sabato zangu walizikufuru daima, nami nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuwaangamiza hukohuko jangwani. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa ambao walishuhudia jinsi nilivyowatoa Waisraeli nchini Misri. Hata hivyo, niliwaapia kulekule jangwani kwamba sitawaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Nilifanya hivyo kwa sababu walizikataa kanuni zangu na kuzikufuru Sabato zangu; kwani walipania kwa moyo sanamu za miungu yao. Lakini nilisalimisha maisha yao, sikuwaangamiza kule jangwani. “Niliwaonya wazawa wao kule jangwani: ‘Msizifuate desturi za wazee wenu, msishike amri zao wala msijitie unajisi kwa kuziabudu sanamu za miungu yao. Mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Fuateni kanuni zangu, shikeni amri zangu kwa uangalifu. Fanyeni Sabato zangu kuwa takatifu, ili ziwe ishara ya agano langu nanyi. Hizo zitawakumbusha kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu.’ “Lakini hata wazawa wao hao waliniasi. Hawakufuata kanuni zangu, hawakushika wala kutekeleza amri zangu ambazo mtu akizishika, huishi. Walizikufuru Sabato zangu. Basi nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao huko jangwani. Lakini nilizuia mkono wangu kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa walioona nikiwatoa nchini Misri. Hata hivyo, niliapa hukohuko jangwani kuwa ningewapeleka katika nchi za mbali na kuwafanya waishi miongoni mwa mataifa ya kigeni, kwa sababu hawakufuata amri zangu, bali walizikataa kanuni zangu, wakazikufuru Sabato zangu na kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao. “Tena niliwapa kanuni mbaya na amri ambazo mtu akizifuata hataishi. Nikawaacha watiwe unajisi kwa tambiko zao za kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu za miungu. Hili lilikuwa pigo lao la adhabu ya kutisha ili watambue kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Sasa, wewe mtu, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Wazee wenu walinikufuru kila mara kwa kukosa uaminifu. Maana nilipowapeleka katika ile nchi niliyoapa kuwapa, kila walipoona kilima kirefu au miti ya majani mengi, walianza kutoa matambiko na tambiko zao na kunichokoza. Hukohuko walitoa tambiko za harufu nzuri na kumimina tambiko za kinywaji. (Mimi nikawauliza, ‘Mahali hapo palipoinuka mnapokwenda panaitwaje?’ Wao wakapaita ‘Mahali palipoinuka’ mpaka leo.) Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawauliza hivi: Je, mtajitia unajisi kwa kufuata desturi za wazee wenu na kuviabudu vitu vinavyonichukiza? Mnapoendelea kutoa tambiko zenu na kuwapitisha watoto wenu motoni mnajitia unajisi mpaka leo hii. Je, nitaulizwa shauri nanyi, enyi watu wa Israeli? Lakini, kama niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba sitakubali kuulizwa shauri nanyi. Nyinyi mnasema mioyoni mwenu, ‘Tutakuwa kama mataifa mengine, kama makabila ya nchi nyingine na kuabudu miti na mawe.’ Hayo mnayopania mioyoni mwenu hayatafanikiwa kamwe. “Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba mimi nitawatawala kwa mkono wenye nguvu, kwa ukali na kuwamwagia ghadhabu yangu. Nitawatoa kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa kwa mkono wangu wenye nguvu, kwa ukali na kwa ghadhabu yangu. Nitawapeleka kwenye jangwa la mataifa; na huko nitawahukumu moja kwa moja. Kama nilivyowahukumu wazee wenu kule jangwani katika nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu nyinyi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitawalazimisha muwe chini ya uchungaji wangu kila mmoja, na kuwafanya mlitii agano langu. Nitaondoa miongoni mwenu waasi na wale wanaonikosea; nitawaondoa katika nchi walikokaa kama wakimbizi, lakini nchi ya Israeli hawataiingia kamwe. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Na sasa, enyi Waisraeli, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Haya! Endeleeni kuziabudu sanamu zenu za miungu, kama hamnisikilizi; lakini mtalazimika kuacha kulikufuru jina langu takatifu kwa tambiko na sanamu zenu. Maana, katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, natamka mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nyinyi nyote watu wa Israeli mtanitumikia huko. Huko mimi nitawapokeeni na kungojea mniletee huko sadaka na tambiko zenu bora na matoleo mliyoyaweka wakfu. Baada ya kuwatoa katika nchi ambako mmetawanywa na kuwakusanya pamoja, nitazipokea tambiko zenu za harufu nzuri. Nami nitadhihirisha utakatifu wangu kati yenu mbele ya mataifa mengine. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowaleta mpaka katika nchi ya Israeli, nchi niliyoapa kuwapa wazee wenu. Huko ndiko mtakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu mabaya ambayo yaliwatieni unajisi; nanyi mtachukizwa kabisa kwa sababu ya maovu yote mliyotenda. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowatendea nyinyi sio kulingana na mwenendo wenu na matendo yenu mabaya, bali kwa heshima ya jina langu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, geukia upande wa kusini uhubiri dhidi ya nchi ya kusini, dhidi ya wakazi wa msitu wa Negebu. Waambie wasikilize neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawasha moto kwako, nao utateketeza miti yote, mibichi na mikavu; utaenea tangu kusini mpaka kaskazini wala hakuna atakayeweza kuzima miali yake. Kila mtu atausikia mchomo wake. Watu wote watajua kwamba ni mimi Mwenyezi-Mungu niliyeuwasha na hautazimika.” Kisha nami nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu! Watu wanalalamika juu yangu na kusema: ‘Huyu akisema, ni mafumbo tu!’”
Ezekieli 20:1-49 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao; uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu; katika siku ile niliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nilijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena niliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao niliwatoa mbele ya macho yao. Tena niliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani. Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao. Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda; zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani. Lakini niliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao niliwatoa. Tena niliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali; kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao. Tena niliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo; nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wametenda kosa juu yangu. Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo niliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifukiza manukato ya kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa. Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo. Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao? Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu; nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika; nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano. Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Nendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu. Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote. Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu. Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si kulingana na njia zenu mbaya, wala si kulingana na matendo yenu maovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu, ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hadi kaskazini zitateketezwa kwa moto huo. Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, wao hunisema; Je! Mtu huyu si mtu mwenye kupiga mithali?
Ezekieli 20:1-49 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao; uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu; katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nalijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao naliwatoa mbele ya macho yao. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani. Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao. Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda; zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani. Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali; kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao. Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo; nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wamekosa kosa juu yangu. Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa. Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo. Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao? Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu; nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika; nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano. Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Enendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu. Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote. Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu. Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si sawasawa na njia zenu mbaya, wala si sawasawa na matendo yenu mabovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu, ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo. Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, wao hunisema; Je! Mtu huyu si mtu mwenye kupiga mithali?
Ezekieli 20:1-49 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema BWANA Mwenyezi.’ “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.” Siku ile niliwaapia kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote. Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.” “ ‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri. Lakini kwa ajili ya Jina langu niliwatoa katika nchi ya Misri. Nilifanya hivyo ili kulinda Jina langu lisinajisiwe machoni mwa mataifa walioishi miongoni mwao, na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli. Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani. Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi BWANA niliwafanya watakatifu. “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani. Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote, kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu, na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao. Lakini niliwahurumia, wala sikuwaangamiza wala kuwafuta kabisa jangwani. Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu; fuateni amri zangu, tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu. Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.” “ ‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani. Lakini nikauzuia mkono wangu, na kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile kingezuia Jina langu kunajisiwa machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba ningewatawanya miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, kwa sababu hawakutii sheria zangu lakini walikuwa wamekataa amri zangu na kuzinajisi Sabato zangu, nayo macho yao yakatamani sanamu za baba zao. Pia niliwaacha wafuate amri ambazo hazikuwa nzuri na sheria ambazo mtu hawezi kuishi kwa hizo sheria. Nikawaacha wanajisiwe kwa matoleo yao ya kuwatoa kafara wazaliwa wao wa kwanza kwa sanamu, ili nipate kuwajaza na hofu hadi wajue kuwa Mimi ndimi BWANA.’ “Kwa hiyo, mwanadamu, sema na watu wa Israeli na uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Katika jambo hili pia, baba zenu walinikufuru kwa kuniacha mimi: Nilipowaleta katika nchi niliyokuwa nimeapa kuwapa na kuona kilima chochote kirefu au mti wowote wenye majani mengi, huko walitoa dhabihu zao, wakatoa sadaka ambazo zilichochea hasira yangu, wakafukiza uvumba wenye harufu nzuri na kumimina sadaka zao za kinywaji. Ndipo nikawaambia: Ni nini maana yake hapa mahali pa juu pa kuabudia mnapopaendea?’ ” (Basi mahali pale panaitwa Bama hata leo.) “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Je, mtajinajisi kama vile baba zenu walivyofanya na kutamani vinyago vyao vya machukizo? Mnapotoa matoleo yenu, yaani kutoa kafara watoto wenu motoni, mnaendelea kujinajisi na sanamu zenu zote hadi leo. Je, niulizwe ushauri na ninyi, ee nyumba ya Israeli? Hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, mimi sitaulizwa ushauri na ninyi. “ ‘Lile lililoko mioyoni mwenu kamwe halitatokea, mnaposema, “Tunataka tuwe kama mataifa mengine, kama watu wengine wa dunia, wanaotumikia miti na mawe.” Hakika kama niishivyo asema BWANA Mwenyezi, nitawatawala kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyooshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika. Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso. Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema BWANA Mwenyezi. Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa agano. Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Kwenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu. Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema BWANA Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote. Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu. Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda. Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowatendea kwa ajili ya Jina langu, wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema BWANA Mwenyezi.’ ” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri dhidi ya upande wa kusini, na utoe unabii dhidi ya msitu wa Negebu. Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Ninakaribia kukuwasha moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo. Kila mmoja ataona kuwa Mimi BWANA ndiye niliyeuwasha huo moto; nao hautazimwa.’ ” Ndipo niliposema, “Aa, BWANA Mwenyezi! Wao hunisema, ‘Huyu si huzungumza mafumbo tu?’ ”