Ezekieli 12:17-28
Ezekieli 12:17-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, kula chakula na kunywa maji yako ukitetemeka kwa hofu. Waambie watu wa nchi hii, kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema juu ya wakazi wa Yerusalemu ambao bado wamo nchini Israeli, kwamba watakula chakula chao kwa hofu na watakunywa maji yao kwa kufadhaika, kwani nchi yao haitakuwa na kitu, kwa sababu kila mkazi ni mdhalimu. Miji yenye watu itateketezwa, na nchi itakuwa ukiwa. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu: Kwa nini methali hii inatajwa katika Israeli: ‘Siku zaja na kupita, lakini maono ya nabii hayatimii?’ Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitakomesha methali hiyo nao hawataitumia tena nchini Israeli. Waambie kuwa wakati umewadia ambapo maono yote yatatimia. Maana hapatakuwa tena na maono ya uongo au kupiga bao miongoni mwa Waisraeli. Mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe nitatangaza yatakayotukia. Nayo yatatukia bila kukawia. Wakati wa uhai wenu, enyi watu waasi, neno nitakalotamka nitalitimiza. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, Waisraeli wanafikiri kwamba maono yako yanahusu siku za baadaye sana, na unabii wako wahusu nyakati za mbali sana! Kwa hiyo waambie, kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kuwa maneno yangu yote yatatimia karibuni. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema!”
Ezekieli 12:17-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, ule chakula chako kwa mtetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana; ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, kuhusu habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake. Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote. Kwa maana hayatakuwapo tena maono yoyote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli. Maana mimi ni BWANA; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 12:17-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, ule chakula chako kwa matetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana; ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake. Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote. Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli. Maana mimi ni BWANA; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 12:17-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, tetemeka unapokula chakula chako, tetemeka kwa hofu unapokunywa maji yako. Waambie watu wa nchi: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi kuhusu wakaaji wa Yerusalemu na katika nchi ya Israeli: Watakula chakula chao kwa wasiwasi na kunywa maji yao kwa kufadhaika, kwa kuwa nchi yao itanyangʼanywa kila kitu chake kwa sababu ya udhalimu wa wote wanaoishi humo. Miji inayokaliwa na watu itaharibiwa na nchi itakuwa ukiwa. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, ni ipi hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia’? Waambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia ambapo kila ono litatimizwa. Kwa maana hapatakuwa tena na maono ya uongo wala ubashiri wa kujipendekeza miongoni mwa watu wa Israeli. Lakini Mimi BWANA nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa kuwa katika siku zako, ewe nyumba ya uasi, nitatimiza kila nisemalo, asema BWANA Mwenyezi.’ ” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, nyumba ya Israeli inasema, ‘Maono yale anayoyaona ni kwa ajili ya miaka mingi ijayo, naye hutabiri kuhusu siku zijazo zilizo mbali.’ “Kwa hiyo, waambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Hakuna maneno yangu yatakayocheleweshwa tena zaidi, lolote nisemalo litatimizwa, asema BWANA Mwenyezi.’ ”