Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 1:1-28

Ezekieli 1:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo siku ya tano ya mwezi wa nne, mwaka wa thelathini, nilikuwa Babuloni kwenye mto Kebari miongoni mwa wale watu waliopelekwa uhamishoni. Basi, mbingu zilifunguka, nikaona maono ya Mungu. Katika siku hiyo ya tano ya mwezi (ulikuwa mwaka wa tano baada ya mfalme Yehoyakini kupelekwa uhamishoni Babuloni), Mwenyezi-Mungu aliongea nami kuhani Ezekieli mwana wa Buzi, nilipokuwa Kaldayo karibu na mto Kebari, naye Mwenyezi-Mungu akaniwekea mkono wake. Nilipotazama niliona upepo wa dhoruba unavuma kutoka kaskazini: Kulikuwa na wingu kubwa lililozungukwa na mngao, na moto ulichomoza humo mfululizo na katikati ya huo moto kulikuwa na kitu kinametameta kama shaba. Kutoka humo nilibainisha viumbe hai wanne, ambao walionekana hivi: Walikuwa na umbo la binadamu. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyoka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Walikuwa na mikono ya binadamu chini ya mabawa yao katika pande zao nne. Ncha za mabawa yao ziligusana kila bawa na bawa lingine. Waliposogea, upande wowote ule, walikwenda mbele moja kwa moja bila kugeuza miili yao. Kuhusu nyuso zao nne kila mmoja wao alikuwa na uso wa binadamu upande wa mbele, uso wa simba upande wa kulia, uso wa ng'ombe upande wa kushoto, na uso wa tai upande wa nyuma. Mabawa mawili ya kila mmoja yalikuwa yamekunjuliwa juu na kugusana na kwa mabawa yale mengine mawili walifunika miili yao. Popote roho ilipotaka kwenda, walikwenda; kila mmoja wao alikwenda mbele moja kwa moja bila kuugeuza mwili wake. Katikati ya hao viumbe hai kulikuwa na kitu kilichoonekana kama makaa yanayowaka moto, kama miali ya moto iliyomulika huku na huko kati ya hao viumbe. Moto huo ulikuwa mwangavu na umeme ulichomoza humo. Viumbe hao pia walikwenda huku na huko kama pigo la umeme. Nilipokuwa nawatazama hao viumbe hai niliona chini karibu na kila kiumbe kulikuwa na gurudumu. Magurudumu hayo yalionekana kuwa ya namna moja, yanametameta kama jiwe la zabarajadi na muundo wao ulikuwa kama gurudumu ndani ya gurudumu lingine. Yaliposogea yalikwenda upande wowote wa pande nne za dira ya dunia bila kugeuka. Mizingo ya hayo magurudumu ilikuwa mirefu kutisha na mizingo ya magurudumu hayo ilikuwa imejaa macho pande zote. Hao viumbe hai walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kandokando yao; na viumbe hao walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu hayo yaliinuka. Popote roho ilipokwenda walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao; maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo. Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda; waliposimama, nayo yalisimama; walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka pamoja nao. Maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo. Juu ya vichwa vya hao viumbe hai kulikuwa na kitu mfano wa anga, kinangaa kama kioo. Chini ya kitu hicho walisimama hao viumbe hai; mabawa mawili ya hao viumbe yalikuwa yamekunjuliwa kuelekeana, na kwa mabawa mengine mawili walifunika miili yao. Walipokuwa wanakwenda, nilisikia sauti ya mabawa yao; sauti ya mvumo huo ilikuwa kama ile ya maji mengi, kama sauti ya ngurumo kutoka kwa Mungu wa majeshi, na kama kelele ya jeshi kubwa. Waliposimama, walikunja mabawa yao. Nilisikia sauti kutoka juu ya kitu kile kama anga kilichokuwa juu ya vichwa vyao. Juu ya kitu hicho niliona kitu kama kiti cha enzi cha johari ya rangi ya samawati. Juu yake aliketi mmoja anayefanana na binadamu. Sehemu ya juu ya mwili wake ilingaa kama shaba, kama moto uliozunguka pande zote; sehemu ya chini ya mwili wake ilikuwa kama moto nayo ilizungukwa na mngao ulioonekana kama upinde wakati wa mvua. Ndivyo ulivyoonekana mfano wa utukufu wa Mwenyezi-Mungu. Nilipouona, nilianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi; mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kulia; na hao wanne walikuwa na uso wa ng'ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda. Kwa habari za kuonekana kwao wale viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya wale viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme. Na wale viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme. Basi, nilipokuwa nikivitazama wale viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha wale viumbe hai, pande zake zote nne. Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine. Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda. Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote. Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa. Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu. Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu. Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao. Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili. Nao walipokwenda nilisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake. Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, niliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote. Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa BWANA. Nami nilipoona nilianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi; mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda. Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme. Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme. Basi, nilipokuwa nikivitazama vile viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha vile viumbe hai, pande zake zote nne. Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine. Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda. Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote. Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa. Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu. Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu. Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao. Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili. Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake. Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote. Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa BWANA. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa miongoni mwa waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu. Katika siku ya tano ya mwezi, mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa BWANA ulikuwa juu yake. Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyongʼaa ndani ya moto. Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu, lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea. Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa hao wanne alikuwa na uso wa mwanadamu, na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, na kwa upande wa kushoto alikuwa na uso wa ngʼombe; pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliokunjuliwa kuelekea juu; kila bawa liligusa bawa la mwenzake kila upande; kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipoenda, walienda pasipo kugeuka. Kuonekana kwa wale viumbe hai kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya wale viumbe; ulikuwa na mwangaza mkali na katika ule moto kulitoka miali ya radi. Wale viumbe walipiga mbio kwenda na kurudi, kama miali ya radi. Nilipokuwa nikitazama wale viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe na nyuso zake nne. Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalimetameta kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilionekana kuwa na gurudumu lingine ndani yake. Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale viumbe; wale viumbe walipoenda, magurudumu hayakugeuka. Kingo za magurudumu zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote. Wale viumbe hai walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea; wakati hao viumbe hai walipoinuka kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka. Popote roho alipoenda, wale viumbe nao walienda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. Viumbe wale waliposogea, nayo magurudumu yalisogea; viumbe waliposimama, nayo pia yalisimama; viumbe walipoinuka juu ya nchi, magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa kuwa roho ya hao viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na la kutisha. Chini ya hiyo nafasi, mabawa yao yalitanda moja kuelekea lingine, na kila mmoja alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. Viumbe wale waliposogea, nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama kishindo cha jeshi. Waliposimama, walishusha mabawa yao. Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa. Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha utawala kulikuwa na umbo, mfano wa mwanadamu. Nikaona kwamba kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea juu, alionekana kama chuma inavyongʼaa ikiwa ndani ya moto, na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto; mwanga wenye kungʼaa sana ulimzunguka. Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mngʼao uliomzunguka. Hivi ndivyo mfano wa utukufu wa BWANA ulionekana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1