Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 9:1-35

Kutoka 9:1-35 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie. Kama ukikataa kuwaacha waondoke na ukiendelea kuwashikilia, nitaunyosha mkono wangu na kuleta maradhi mabaya sana juu ya mifugo yenu yote: Ng'ombe, farasi, punda, ngamia, mbuzi na kondoo. Na, nitaitenganisha mifugo ya Waisraeli na mifugo ya Wamisri ili mnyama hata mmoja wa Waisraeli asife.’” Tena, Mwenyezi-Mungu akaweka wakati maalumu akisema, “Kesho mimi Mwenyezi-Mungu nitatekeleza jambo hilo nchini Misri.” Kesho yake Mwenyezi-Mungu akafanya alichosema. Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna mnyama hata mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Farao akauliza habari juu ya wanyama wa Waisraeli, akaambiwa kuwa hakuna mnyama wao hata mmoja aliyekufa. Hata hivyo, Farao akabaki mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni kila mmoja wenu magao ya majivu ya tanuri, kisha Mose ayarushe juu hewani mbele ya Farao. Majivu hayo yatakuwa vumbi nyembamba itakayoenea juu ya nchi yote ya Misri. Yatasababisha majipu yatakayotumbuka na kuwa vidonda kwa watu na wanyama kila mahali nchini Misri.” Basi, wakachukua majivu kutoka kwenye tanuri, wakamwendea Farao, naye Mose akayarusha juu hewani. Watu na wanyama wakavamiwa na majipu hata wale wachawi hawakuweza kujitokeza maana wao pamoja na Wamisri wote pia walivamiwa na majipu hayo. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwasikiliza kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho, amka alfajiri na mapema umwendee Farao, umwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie. Maana safari hii, wewe mwenyewe, maofisa wako na watu wako mtakumbana na mapigo yangu makali. Nawe utatambua kwamba hakuna yeyote duniani aliye kama mimi. Ningalikwisha kukuangamiza tayari wewe na watu wako kwa maradhi mabaya, nanyi mngalikuwa mmekwisha angamia. Lakini nimewaacheni muishi ili kudhihirisha uwezo wangu. Kwa hiyo dunia yote itatambua kuwa mimi ni nani. Lakini bado unaonesha kiburi dhidi ya watu wangu, wala huwaachi waondoke. Kwa hiyo kesho, wakati kama huu, nitaleta mvua kubwa ya mawe ambayo haijawahi kutokea nchini Misri, tangu mwanzo wake hadi leo. Kwa hiyo agiza mifugo yako na chochote kilicho huko mashambani viwekwe mahali salama; kwa maana mvua ya mawe itamnyeshea kila mtu na mnyama aliye shambani na ambaye hayuko nyumbani; wote watakufa.’” Baadhi ya maofisa wa Farao waliyatia maanani maneno hayo ya Mwenyezi-Mungu, wakawapeleka watumwa na wanyama wao nyumbani mahali pa usalama. Lakini yule ambaye hakulijali neno la Mwenyezi-Mungu aliwaacha watumwa wake na wanyama wake mashambani. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni, ili mvua ya mawe inyeshe kila mahali nchini Misri. Imnyeshee mtu, mnyama na kila mmea shambani.” Basi, Mose alinyosha fimbo yake kuelekea mbinguni. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta mvua ya mawe na ngurumo; umeme ukaipiga nchi. Mwenyezi-Mungu alinyesha mvua ya mawe nchini Misri, mvua kubwa ya mawe iliyoandamana na mfululizo wa umeme, ambayo hakuna mwananchi yeyote wa Misri aliyepata kamwe kushuhudia kabla. Mvua hiyo ya mawe ilivunjavunja kila kitu katika mashamba na kila mahali nchini Misri: Wanyama na watu. Mawe ya mvua yakavunjavunja mimea yote na miti mashambani. Jambo hilo lilifanyika kote nchini Misri isipokuwa tu sehemu ya Gosheni walimokaa Waisraeli; humo haikuwako mvua ya mawe. Basi, Farao akaagiza Mose na Aroni waitwe, akawaambia, “Safari hii nimetenda dhambi. Mwenyezi-Mungu ana haki; mimi na watu wangu tumekosa. Mwombeni Mwenyezi-Mungu kwani ngurumo hii na mvua ya mawe vimezidi. Mimi nitawaacheni mwondoke na wala hamtakaa tena zaidi.” Mose akamwambia, “Mara tu nitakapotoka nje ya mji nitainua mikono na kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ngurumo itakoma na hakutakuwa na mvua ya mawe tena ili utambue kwamba dunia ni yake Mwenyezi-Mungu. Lakini najua kwamba wewe na maofisa wako bado hammwogopi Mwenyezi-Mungu.” (Kitani na mimea ya shayiri vyote vilikuwa vimeharibiwa, kwa sababu shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua. Lakini ngano na jamii nyingine ya ngano havikuharibiwa kwa kuwa hiyo huchelewa kukomaa). Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akatoka nje ya mji. Kisha akainua mikono yake kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ngurumo na mvua ya mawe vikakoma; mvua ikaacha kunyesha duniani. Lakini Farao alipoona kuwa mvua ya mawe na ngurumo vimekoma, aliirudia dhambi yake tena, akawa mkaidi, yeye pamoja na maofisa wake. Basi, kama Mwenyezi-Mungu alivyombashiria Mose, Farao alikaidi akakataa kuwaruhusu Waisraeli waondoke.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:1-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, yuasema, Wape ruhusa watu wangu ili waende wanitumikie. Kwani ukikataa kuwapa ruhusa waende, na kuzidi kuwazuia, tazama, mkono wa BWANA uko juu ya wanyama wako wa mifugo walioko kondeni, juu ya farasi, na juu ya punda, na juu ya ngamia, na juu ya ng'ombe, na juu ya kondoo; kutakuwa na tauni nzito sana. Kisha BWANA atawatenga wanyama wa Israeli na wanyama wa Misri; wala hakitakufa kitu chochote cha wana wa Israeli. Naye BWANA akaweka muda, akasema, Kesho BWANA atalifanya jambo hili katika nchi. BWANA akalifanya jambo hilo siku ya pili, na wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa; lakini katika wanyama wa wana wa Israeli hakufa hata mmoja. Farao akatuma watu, na tazama, hapana mmoja aliyekufa katika wanyama wa wana wa Israeli. Lakini moyo wa Farao ulikuwa mzito, wala hakuwapa hao watu ruhusa waende zao. BWANA akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuri, kisha Musa ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao. Nayo yatakuwa ni mavumbi membamba juu ya nchi yote ya Misri, nayo yatakuwa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama, katika nchi yote ya Misri. Basi wakatwaa majivu ya tanuri, na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa ni majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo. BWANA akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyomwambia Musa. BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni kote. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu ii hii, ili nikuoneshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma watu wahimize kuingiza ndani mifugo yako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe. Farao akatuma watu, na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, Mimi nimekosa wakati huu; BWANA ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu. Mwombeni BWANA; kwa kuwa zimekuwa za kutosha ngurumo hizo kuu na hii mvua ya mawe; nami nitawapa ninyi ruhusa mwende zenu, msikae zaidi. Musa akamwambia, Mara nitakapotoka mjini nitamwinulia BWANA mikono yangu; na hizo ngurumo zitakoma, wala haitanyesha mvua ya mawe tena; ili upate kujua ya kuwa dunia hii ni ya BWANA. Lakini, wewe na watumishi wako, najua ya kuwa ninyi hamtamcha BWANA Mungu bado. Kitani na shayiri zilipigwa; maana shayiri zilikuwa na masuke na kitani zilikuwa katika kutoa maua. Lakini ngano na kusemethi hazikupigwa; maana, zilikuwa hazijakua bado. Musa akatoka mjini, kutoka kwa Farao, akamwinulia BWANA mikono yake; na zile ngurumo na ile mvua ya mawe zikakoma, wala mvua haikunyesha juu ya nchi. Farao alipoona ya kwamba mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akazidi kufanya dhambi, na kuufanya moyo wake mzito, yeye na watumishi wake. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu naye hakuwapa wana wa Israeli ruhusa waende zao; kama BWANA alivyonena kwa kinywa cha Musa.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:1-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, yuasema, Wape ruhusa watu wangu ili waende wanitumikie. Kwani ukikataa kuwapa ruhusa waende, na kuzidi kuwazuia, tazama, mkono wa BWANA u juu ya wanyama wako wa mifugo walioko kondeni, juu ya farasi, na juu ya punda, na juu ya ngamia, na juu ya ng’ombe, na juu ya kondoo; kutakuwa na tauni nzito sana. Kisha BWANA atawatenga wanyama wa Israeli na wanyama wa Misri; wala hakitakufa kitu cho chote cha wana wa Israeli. Naye BWANA akaweka muda, akasema, Kesho BWANA atalifanya jambo hili katika nchi. BWANA akalifanya jambo hilo siku ya pili, na wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa; lakini katika wanyama wa wana wa Israeli hakufa hata mmoja. Farao akatuma watu, na tazama, hapana mmoja aliyekufa katika wanyama wa wana wa Israeli. Lakini moyo wa Farao ulikuwa mzito, wala hakuwapa hao watu ruhusa waende zao. BWANA akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuuni, kisha Musa na ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao. Nayo yatakuwa ni mavumbi membamba juu ya nchi yote ya Misri, nayo yatakuwa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama, katika nchi yote ya Misri. Basi wakatwaa majivu ya tanuuni, na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa ni majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo. BWANA akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyomwambia Musa. BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe. Farao akatuma watu, na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, Mimi nimekosa wakati huu; BWANA ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu. Mwombeni BWANA; kwa kuwa zimekuwa za kutosha ngurumo hizo kuu na hii mvua ya mawe; nami nitawapa ninyi ruhusa mwende zenu, msikae zaidi. Musa akamwambia, Mara nitakapotoka mjini nitamwinulia BWANA mikono yangu; na hizo ngurumo zitakoma, wala haitanyesha mvua ya mawe tena; ili upate kujua ya kuwa dunia hii ni ya BWANA. Lakini, wewe na watumishi wako, najua ya kuwa ninyi hamtamcha BWANA Mungu bado. Kitani na shayiri zilipigwa; maana shayiri zilikuwa na masuke na kitani zilikuwa katika kutoa maua. Lakini ngano na kusemethu hazikupigwa; maana, zilikuwa hazijakua bado. Musa akatoka mjini, kutoka kwa Farao, akamwinulia BWANA mikono yake; na zile ngurumo na ile mvua ya mawe zikakoma, wala mvua haikunyesha juu ya nchi. Farao alipoona ya kwamba mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akazidi kufanya dhambi, na kuufanya moyo wake mzito, yeye na watumishi wake. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu naye hakuwapa wana wa Israeli ruhusa waende zao; kama BWANA alivyonena kwa kinywa cha Musa.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:1-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo BWANA, Mungu wa Waebrania, asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.” Usipowaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia, mkono wa BWANA utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ngʼombe wako, kondoo na mbuzi. Lakini BWANA ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ” BWANA akaweka wakati na kusema, “Kesho BWANA atalitenda hili katika nchi.” Siku iliyofuata BWANA akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende. Kisha BWANA akamwambia Musa na Haruni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Musa ayarushe angani mbele ya Farao. Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura kwenye miili ya watu na ya wanyama katika nchi yote.” Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Musa akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea kwenye miili ya watu na ya wanyama. Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya majipu yaliyokuwa kwenye miili yao, na kwenye miili ya Wamisri wote. Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile BWANA alivyokuwa amemwambia Musa. Kisha BWANA akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili waweze kuniabudu, au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama mimi duniani kote. Kwa kuwa hadi sasa ningekuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nikuoneshe uwezo wangu, na jina langu litangazwe duniani kote. Bado unaendelea kujiinua dhidi ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. Hivyo basi, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa hadi leo. Sasa toa amri mifugo yako na kila kitu ulicho nacho shambani, kipelekwe mahali pa usalama. Kwa sababu mvua ya mawe itamwangukia kila mtu na mnyama ambaye hajaletwa ndani, na ambaye bado yuko nje shambani; nao watakufa.’ ” Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la BWANA wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani. Lakini wale waliopuuza neno la BWANA wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani. Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili mvua ya mawe inyeshe Misri yote: juu ya watu, wanyama, na juu ya kila kitu kinachoota katika mashamba ya Misri.” Musa alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, BWANA akatuma ngurumo na mvua ya mawe; mwanga wa radi ukamulika hadi nchi. Kwa hiyo BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi ya Misri; mvua ya mawe ikanyesha, na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha zaidi, ambayo haijawahi kutokea katika Misri tangu nchi hiyo iwe taifa. Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba: watu na wanyama; ikaharibu kila kitu kilichoota mashambani na kungʼoa kila mti. Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. BWANA ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji. Mwombeni BWANA, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kutosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.” Musa akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba BWANA. Ngurumo zitakoma na hapatakuwa mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa nchi ni mali ya BWANA. Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi BWANA Mungu.” (Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua. Hata hivyo, ngano na kusemethi hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa.) Kisha Musa akaondoka kwa Farao, akaenda nje ya mji. Musa akanyoosha mikono yake kuelekea kwa BWANA, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini. Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu. Kwa hiyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile BWANA alivyokuwa amesema kupitia Musa.

Shirikisha
Soma Kutoka 9