Kutoka 7:7-13
Kutoka 7:7-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose alikuwa na umri wa miaka themanini, na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu wakati huo walipoongea na Farao. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambieni mthibitishe jambo hilo kwa kutenda miujiza, wewe utamwambia Aroni aichukue fimbo yake, aitupe mbele ya Farao, nayo itakuwa nyoka.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kufanya kama walivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aroni aliitupa fimbo yake chini mbele ya Farao na maofisa wake, nayo ikawa nyoka. Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao. Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 7:7-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo hivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wajuzi na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
Kutoka 7:7-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
Kutoka 7:7-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Musa alikuwa na umri wa miaka themanini na Haruni alikuwa na umri wa miaka themanini na tatu walipozungumza na Farao. BWANA akamwambia Musa na Haruni, “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Haruni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.” Ndipo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakafanya sawasawa na jinsi BWANA alivyoagiza. Haruni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Misri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Haruni ikazimeza zile fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema.