Kutoka 7:1-7
Kutoka 7:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tazama, mimi nakufanya kuwa kama mungu kwa Farao, naye ndugu yako Aroni atakuwa nabii wako. Utamwambia ndugu yako Aroni mambo yote nitakayokujulisha, naye Aroni nduguyo, atamwambia Farao awaache Waisraeli watoke nchini mwake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Na hata kama nitazidisha miujiza na maajabu yangu katika nchi ya Misri, Farao hatakusikiliza, na hapo nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuiadhibu vikali nchi ya Misri, na kuwatoa watu wangu, makabila ya Israeli, kutoka Misri. Nitafanya hivyo kwa matendo makuu ya hukumu dhidi ya Misri. Wakati nitakapounyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Misri na kuwatoa Waisraeli miongoni mwao. Ndipo Wamisri watakapotambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakafanya hivyo; naam, walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini, na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu wakati huo walipoongea na Farao.
Kutoka 7:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo hivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao.
Kutoka 7:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao.
Kutoka 7:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Tazama, nimekufanya kama Mungu kwa Farao, naye Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako. Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Haruni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri, hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikosi vyangu, watu wangu Waisraeli. Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi BWANA nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli humo.” Musa na Haruni wakafanya sawasawa na jinsi BWANA alivyowaamuru. Musa alikuwa na umri wa miaka themanini na Haruni alikuwa na umri wa miaka themanini na tatu walipozungumza na Farao.