Kutoka 7:1-25
Kutoka 7:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tazama, mimi nakufanya kuwa kama mungu kwa Farao, naye ndugu yako Aroni atakuwa nabii wako. Utamwambia ndugu yako Aroni mambo yote nitakayokujulisha, naye Aroni nduguyo, atamwambia Farao awaache Waisraeli watoke nchini mwake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Na hata kama nitazidisha miujiza na maajabu yangu katika nchi ya Misri, Farao hatakusikiliza, na hapo nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuiadhibu vikali nchi ya Misri, na kuwatoa watu wangu, makabila ya Israeli, kutoka Misri. Nitafanya hivyo kwa matendo makuu ya hukumu dhidi ya Misri. Wakati nitakapounyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Misri na kuwatoa Waisraeli miongoni mwao. Ndipo Wamisri watakapotambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakafanya hivyo; naam, walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini, na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu wakati huo walipoongea na Farao. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambieni mthibitishe jambo hilo kwa kutenda miujiza, wewe utamwambia Aroni aichukue fimbo yake, aitupe mbele ya Farao, nayo itakuwa nyoka.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kufanya kama walivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aroni aliitupa fimbo yake chini mbele ya Farao na maofisa wake, nayo ikawa nyoka. Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao. Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Moyo wa Farao umekuwa mgumu. Anakataa kuwaacha Waisraeli waondoke. Basi, nenda ukakutane naye kesho asubuhi, wakati anapokwenda mtoni Nili. Mngojee kando ya mto. Chukua mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka. Kisha mwambie hivi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma kwako, naye asema hivi, ‘Waache watu wangu waende zao ili wanitumikie jangwani, lakini mpaka sasa wewe hupendi kutii. Basi, Mwenyezi-Mungu asema kwamba sasa utamtambua yeye ni nani. Nitayapiga maji ya mto Nili kwa fimbo hii, na maji yote yatageuka kuwa damu. Samaki waliomo mtoni Nili watakufa, mto wote utanuka vibaya, na Wamisri watachukia kabisa kunywa maji yake.’” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni aichukue fimbo yake na kuinyosha juu ya maji ya Misri, juu ya mito yote, mifereji, madimbwi na mabwawa yao yote, nayo yatakuwa damu. Kutakuwa na damu nchini kote, na hata katika vyombo vyote vya mbao na vya mawe.” Mose na Aroni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Aroni aliinua fimbo yake juu mbele ya Farao na maofisa wake, akayapiga maji ya mto Nili, na maji yote mtoni yakageuka kuwa damu. Samaki wakafa, mto ukanuka vibaya sana hata Wamisri wasiweze kunywa maji yake. Nchi nzima ikajaa damu. Lakini wachawi wa Misri kwa kutumia uchawi wao wakafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo moyo wa Farao ukabaki kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni; ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema. Basi, Farao akarudi nyumbani kwake, na hata haya yaliyotokea hakuyajali. Wamisri wote wakachimbachimba kandokando ya mto Nili ili wapate maji ya kunywa, kwani hawakuweza kunywa maji ya mto huo. Pigo hilo la mto Nili lilidumu siku saba.
Kutoka 7:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo hivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo hivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wajuzi na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena. BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote ya Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena. Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. Wamisri wote wakachimbachimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. Zikatimia siku saba, baada ya BWANA kuupiga ule mto.
Kutoka 7:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena. BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena. Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. Wamisri wote wakachimba-chimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. Zikatimia siku saba, baada ya BWANA kuupiga ule mto.
Kutoka 7:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Tazama, nimekufanya kama Mungu kwa Farao, naye Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako. Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Haruni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri, hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikosi vyangu, watu wangu Waisraeli. Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi BWANA nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli humo.” Musa na Haruni wakafanya sawasawa na jinsi BWANA alivyowaamuru. Musa alikuwa na umri wa miaka themanini na Haruni alikuwa na umri wa miaka themanini na tatu walipozungumza na Farao. BWANA akamwambia Musa na Haruni, “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Haruni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.” Ndipo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakafanya sawasawa na jinsi BWANA alivyoagiza. Haruni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Misri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Haruni ikazimeza zile fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Kisha BWANA akamwambia Musa, “Moyo wa Farao ni mgumu; anakataa kuwaacha watu waondoke. Nenda kwa Farao asubuhi anapoenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Mto Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. Kisha umwambie, ‘BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. Hili ndilo asemalo BWANA: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi BWANA: Kwa fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga maji ya Mto Naili, nayo yatabadilika kuwa damu. Samaki walio katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya; Wamisri hawataweza kunywa maji yake.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.” Musa na Haruni wakafanya kama vile BWANA alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri. Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni. Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto. Zilipita siku saba baada ya BWANA kuyapiga maji ya Mto Naili.