Kutoka 5:4-14
Kutoka 5:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini mfalme wa Misri akawajibu, “Enyi Mose na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.” Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!” Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema, “Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia. Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’ Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.” Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi. Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’” Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.” Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?”
Kutoka 5:4-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Nendeni zenu kwa mizigo yenu. Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. Nendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya takataka ya mashamba badala ya majani. Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza?
Kutoka 5:4-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu. Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka ya mashamba badala ya majani. Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza?
Kutoka 5:4-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Musa na Haruni mnawaondoa watu kutoka kwenye kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!” Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.” Siku hiyo hiyo, Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu, akawaambia: “Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali; wakusanye nyasi zao wenyewe. Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’ Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.” Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa nyasi tena. Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ” Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi. Viongozi wa watumwa wakasisitiza wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.” Wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”