Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 4:1-31

Kutoka 4:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Mose akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Unashika nini mkononi mwako?” Mose akamwambia, “Fimbo.” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Mose akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Mose akaikimbia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Mose akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.” Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Mose akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji. Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Mose akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake. Mungu akamwambia Mose, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili. Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Ewe Bwana wangu, mimi sina ufasaha wa kuongea tangu zamani; hata baada ya wewe kusema nami mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu? Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi? Aone au awe kipofu? Je, si mimi Mwenyezi-Mungu? Basi, nenda! Mimi nitakiongoza kinywa chako na kukufundisha cha kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana wangu, tafadhali nakusihi, umtume mtu mwingine.” Ndipo hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Je, si yuko ndugu yako Aroni ambaye ni Mlawi? Najua yeye ana ufasaha wa kuongea. Tena anakuja kukutana nawe, na mara tu atakapokuona atafurahi moyoni. Wewe utaongea naye na kumwambia yote atakayosema. Mimi nitawasaidieni na kuwafundisha mambo mtakayofanya. Aroni ataongea na Waisraeli kwa niaba yako. Yeye atakuwa msemaji wako, nawe utakuwa kama Mungu kwake. Utaichukua mkononi mwako fimbo hii ambayo utaitumia kufanya zile ishara.” Mose alirudi kwa Yethro, baba mkwe wake, akamwambia, “Tafadhali niruhusu nirudi Misri kwa ndugu zangu, nikaone kama bado wako hai.” Yethro akamwambia, “Nenda kwa amani.” Mose akiwa bado nchini Midiani, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi Misri kwa sababu wale wote waliotaka kukuua wamekwisha kufa.” Basi, Mose akamchukua mkewe na watoto wake, akawapandisha juu ya punda, akaanza safari ya kurudi Misri. Mkononi mwake alichukua ile fimbo aliyoamriwa na Mungu aichukue. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo kuifanya. Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachia Waisraeli waondoke. Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume! Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamuua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.’” Akiwa bado njiani kurudi Misri, Mose alikuwa mahali pa kulala wageni; basi, Mungu alikutana naye na kutaka kumuua. Hapo Zipora akakimbia haraka, akachukua jiwe kali, akalikata govi la mwanawe na kumgusa nalo Mose miguuni akisema, “Wewe ni bwana harusi wa damu”. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwacha Mose. Zipora alikuwa amesema, “Bwana harusi wa damu,” kwa sababu ya kutahiri. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukakutane na Mose.” Basi, Aroni akaenda, akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Naye Mose akamwambia Aroni maneno yote aliyoambiwa na Mwenyezi-Mungu ayaseme, na miujiza yote aliyoagizwa atende. Kisha Mose na Aroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli. Aroni akawaambia maneno yote Mwenyezi-Mungu aliyokuwa amemwagiza Mose, na kuifanya ile miujiza mbele ya watu wote. Watu wakaamini. Na waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu amewajia kuwasaidia Waisraeli, na kwamba ameyaona mateso yao, wote wakainamisha vichwa vyao na kumwabudu.

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia kutoka mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, nenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara. Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, rudi Misri; kwa kuwa wale watu wote walioutaka uhai wako wamekwisha kufa. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. Ndipo walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye, akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu lenye makali na kulikata govi ya zunga la mwanawe, na kulibwaga miguuni pa Musa akasema. Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainamisha vichwa vyao wakasujudu.

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara. Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Musa akamjibu, “Itakuwaje wasiponiamini au kunisikiliza, waseme, ‘BWANA hakukutokea’?” Ndipo BWANA akamuuliza, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akamjibu, “Ni fimbo.” BWANA akasema, “Itupe chini.” Musa akaitupa fimbo chini, nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. Kisha BWANA akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate kwenye mkia.” Basi Musa akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. BWANA akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa BWANA, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.” Kisha BWANA akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Musa akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Musa akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake. Ndipo BWANA akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.” Musa akamwambia BWANA, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha hapo awali, wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.” BWANA akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu uwezo wa kuona au upofu? Je, si mimi, BWANA? Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.” Lakini Musa akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.” Ndipo hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Musa, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Haruni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. Haruni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.” Kisha Musa akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.” Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.” Basi BWANA alikuwa amemwambia Musa huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili asiwaruhusu watu waende. Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu aende; basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ” Musa alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, BWANA akakutana naye, akataka kumuua. Lakini Sipora akachukua kisu cha gumegume, akakata govi la mwanawe na kugusa miguu ya Musa nalo. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” (Sipora alipomwita Musa, “Bwana arusi wa damu”, alikuwa anamaanisha ile tohara.) Baada ya hayo BWANA akamwacha. BWANA akamwambia Haruni, “Nenda jangwani ukamlaki Musa.” Basi akakutana na Musa kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Kisha Musa akamwambia Haruni kila kitu BWANA alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya. Musa na Haruni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, naye Haruni akawaambia kila kitu BWANA alichokuwa amemwambia Musa. Pia akafanya ishara mbele ya watu, nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa BWANA anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.

Shirikisha
Soma Kutoka 4