Kutoka 39:1-43
Kutoka 39:1-43 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa kutumia sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu walifuma sare za kuvaa wakati wa kuhudumu mahali patakatifu. Walimshonea Aroni mavazi matakatifu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Walitengeneza kizibao kwa nyuzi za dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. Waliifua dhahabu na kuikata katika nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa kwa ustadi. Kizibao hicho kilivaliwa kwa kamba mbili mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. Mkanda uliofumwa kwa ustadi juu yake ili kuifungia ulikuwa kitu kimoja na kizibao hicho, na ulitengenezwa kwa vitu hivyohivyo: Dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha waliandaa vito vya sardoniki na kuvipanga katika vijalizo vya dhahabu; navyo vilichorwa, kama mtu achoravyo mhuri, majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Waliviweka vito hivyo katika kanda za mabegani za kile kizibao ili kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mafundi walitengeneza kifuko cha kifuani kama vile walivyokitengeneza kile kizibao, kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, rangi zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, sentimita 22 kwa sentimita 22 nacho kilikunjwa. Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za mawe ya thamani; safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; safu ya pili ilikuwa ya zumaridi, na johari ya rangi ya samawati na almasi; safu ya tatu ilikuwa ya yasintho, ya akiki nyekundu na amethisto; na safu ya nne ilikuwa ya zabarajadi, ya shohamu na yaspi; yote yalimiminiwa vijalizo vya dhahabu. Basi, palikuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Yalikuwa yamechorwa kama wachoravyo mhuri, kila moja limechorwa jina kuwakilisha makabila kumi na mawili. Walikitengenezea kile kifuko cha kifuani mikufu ya dhahabu safi. Walitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu safi na pete mbili za dhahabu, na kuzitia pete hizo kwenye ncha mbili za juu za kifuko hicho. Mikufu hiyo miwili ya dhahabu waliifunga kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. Zile ncha mbili za mikufu ya dhahabu walizitia kwenye vile vijalizo viwili wakazishikamanisha na vile vipande viwili vya mabegani vya kizibao, upande wa mbele. Walitengeneza pete mbili za dhahabu, wakazitia penye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko hicho cha kifuani karibu na kizibao. Walitengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kinapoungana na ule mkanda uliofumwa kwa ustadi. Walifunga kifuko cha kifuani kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Alitengeneza kanzu ya kuvaa ndani ya kizibao ya rangi ya buluu. Joho hilo lilikuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, nayo ilizungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. Kwenye upindo wa chini wa kanzu walifuma mapambo ya makomamanga ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. Kisha walitengeneza njuga za dhahabu, na kila baada ya komamanga walitia njuga kwenye upindo wa joho. Hivyo, njuga na komamanga vilifuatana kuuzunguka upindo wa joho hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha wakawafumia Aroni na wanawe vizibao vya kitani safi, kilemba cha kitani safi, kofia za kitani safi, suruali za kitani safi iliyosokotwa, na mikanda ya kitani safi iliyosokotwa kwa sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu na kuitarizi vizuri, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake; kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu, sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema; meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu; kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo; madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema; madhabahu ya shaba na wavu wake wa shaba, mipiko yake na vyombo vyake vyote; bakuli, birika na tako lake; vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake; pazia la mlango wa ua, kamba zake na vigingi vyake; vyombo vyote vilivyohitajika katika huduma ya hema takatifu, yaani hema la mkutano; na mavazi yote yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni, na ya wanawe kwa ajili ya huduma ya ukuhani. Waisraeli walifanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mose alikagua kila kitu, akaridhika kwamba walikuwa wamefanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hivyo Mose akawabariki.
Kutoka 39:1-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na zile nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyatengeneza hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana. Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili. Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake mhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli. Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa. Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza. Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi. Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto. Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake. Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora mihuri, kila moja kwa jina lake, kwa yale makabila kumi na mawili. Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi. Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko. Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko. Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi. Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawati, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akafanya hilo joho la naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawati yote; na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke. Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawati, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa. Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga; njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa, na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakafanya hilo bamba la hilo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa mhuri, MTAKATIFU KWA BWANA. Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawati ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya. Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na vitako yake; na kifuniko chake cha ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara; na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema; na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho; na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa, na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema; na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake; na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na vitako vyake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania, na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani. Sawasawa na yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli. Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama BWANA alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo hivyo; basi Musa akawaombea heri.
Kutoka 39:1-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na zile nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyafanya hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana. Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili. Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake muhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli. Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa. Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza. Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi. Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto. Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake. Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora muhuri, kila moja kwa jina lake, kwa zile kabila kumi na mbili. Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi. Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko. Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko. Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi. Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote; na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke. Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa. Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga; njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa, na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Nao wakafanya hilo bamba la hiyo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa muhuri, MTAKATIFU KWA BWANA. Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawi ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa. Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya. Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake; na kifuniko chake cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara; na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema; na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho; na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa, na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema; na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na matako yake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania, na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani. Sawasawa na yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli. Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama BWANA alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo; basi Musa akawaombea heri.
Kutoka 39:1-43 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Haruni mavazi matakatifu, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Akatengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kitani iliyosokotwa vizuri. Akafua vipande vyembamba vya dhahabu kwa nyundo na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi. Akatengeneza vipande vya mabegani vya kizibau, vilivyounganishwa kwenye pembe zake mbili kwa ajili ya kufungia. Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho: ulikuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao ulitengenezwa kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Akatengeneza vito vya shohamu vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa na majina ya wana wa Israeli kama vile muhuri huchorwa. Kisha akavifungia kwenye vipande vya mabega ya kizibau kuwa vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Akatengeneza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili. Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi; safu ya pili ilikuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi; safu ya tatu ilikuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto; katika safu ya nne ilikuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo vilitiwa kwenye vijalizo vya dhahabu. Kulikuwa na vito kumi na viwili, kimoja kwa kila jina la wana wa Israeli; kila kimoja kilichorwa kama muhuri kwa jina mojawapo la makabila yale kumi na mawili. Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani alitengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba. Akatengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani. Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani, nazo zile ncha nyingine za mkufu akazifunga kwenye vile vijalizo viwili, na kuziunganisha na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele. Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuziunganisha kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau. Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuziunganisha sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau. Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kizibau kwa kamba ya buluu, wakiziunganisha na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Akashona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, kazi ya mfumaji, na lilikuwa na nafasi ya shingo katikati ya joho lile iliyofanana na ukosi, na utepe ulioshonwa kuizunguka nafasi hiyo ili isichanike. Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho. Kisha akatengeneza vikengele vya dhahabu safi na kuviunganisha kuzunguka pindo hilo kati ya hayo makomamanga. Hivyo vikengele na makomamanga vilipishana kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Pia akamtengenezea Haruni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji, na kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani, na nguo za ndani za kitani iliyosokotwa vizuri. Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, na zambarau, na nyekundu, kazi ya mtarizi, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Kisha akatengeneza lile bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa BWANA. Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kuliunganisha na kile kilemba, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Kwa hiyo kazi yote ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa na jinsi BWANA alivyomwagiza Musa. Ndipo wakaleta maskani ya Mungu kwa Musa: hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake; kifuniko cha ngozi za kondoo dume kilichotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la kufunikia; Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema, meza pamoja na vyombo vyake vyote, na mikate ya Wonesho; kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote, pamoja na mafuta kwa ajili ya taa; madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri, na pazia la ingilio la hema; madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote, sinia, na tako lake; mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na pazia la ingilio la ua; kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua; vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania; na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Haruni na mavazi ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani. Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vile BWANA alivyokuwa amemwagiza Musa. Musa akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa na jinsi BWANA alivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Musa akawabariki.